Monday, 1 September 2014

WAFANYAKAZI WA JOHNSON GROUP KESHO SEPTEMBA 2 WATAANDAMANA HADI KWA MKUU WA MKOA KUMSHITAKI MWAJIRI WAO

Baadhi ya wafanyakazi wanaomlalamikia mkurugenzi wa Kampuni ya Johnson Group, Gareth Johnson wakiwa wamezingira lango la kuingilia ofisi za kampuni hiyo Kitwiru mjini Iringa
lango la kati la kuingilia ofisi hizo
Sehemu ya yadi ya kampuni hiyo
Meneja wa tawi wa kampuni hiyo, Leonard Lukule
WAFANYAKAZI zaidi ya 40  wa kampuni inayokodisha mitambo ya kutengeneza barabara ya Johnson Group kesho saa mbili na nusu asubuhi wameahidi kuandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Iringa wakiwa na malalamiko kibao dhidi ya mwajiri wao.

Ofisi za Kampuni hiyo iliyoingia mjini Iringa mwaka 2009 ikitokea jijini Dar es Salaam zipo eneo la Kitwiru katika yadi ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Piri Mohamed, mbele kidogo ya kituo cha kuuza mafuta cha kampuni ya Asas barabara ya Iringa Mbeya.

Wafanyakazi hao wanadai kunyanyaswa na Gareth Johnson waliyesema ndiye Mkurugenzi wa kampuni hiyo.

Wamesema mbali na kulipwa mishahara kiduchu ya kati ya Sh 80,000 na Sh270,000 kwa kazi ngumu wanayofanya na kampuni hiyo, mwajiri wao huyo hawasilishi michango yao kwa shirika la hifadhi ya jamii la PPF ambalo wao ni wanachama wake.

Muhutasari wa ripoti ya michango hiyo ya mmoja wa wafanyakazi hao, Idd Salehe inaonesha kwa mara ya mwisho mwajiri huyo kuwasilisha michango yao ilikuwa Mei, 2008.

Salehe alisema wakati huo alikuwa akilipwa mshahara wa Sh 180,390 na mchango wake PPF ulikuwa Sh 18,039 huku mwajiri wake akimchangia kiasi kama hicho.

“Tangu wakati huo hajawahi kuwasilisha michango hiyo japokuwa katika mishahara yetu anaendelea kutukata michango hiyo,” alisema.

Baada ya kugundua wananyanyaswa na mwajiri wao huyo, wafanyakazi hao wamezitaka taasisi zinazohusika na ajira kuingilia kati ili kujua kama wanacholipwa ni stahiki yao kwa mujibu wa sheria na kumlazimisha mwajiri huyo kuwalipa madai yao yote kabla ya kuwalipa mafao yao kwakuwa hawataki tena kuendelea na mikataba yao ya kazi.

Kwa kile kilichoelezwa na wafanyakazi hao na kuthibitishwa na Meneja wa Kampuni hiyo, tawi la Iringa, Leonard Lukule, wafanyakazi hao walipumzishwa kazi miezi minne iliyopita japokuwa wanaendelea kulipwa mishara yao ya kila mwezi.

“Kampuni iko katika hali mbaya kifedha kwasababu haipati kazi za kutosha kwa muda mrefu sasa, mitambo yetu mingi tulikuwa tunakodisha kwa kampuni ya Aarseleff-Interbeton J.V iliyokuwa inajenga barabara ya Iyovi Iringa, Iringa Mafinga na Sumbawanga," alisema.

Alisema pamoja na kuendelea kuwalipa mishahara kampuni imefikia maamuzi ya kuvunja mikataba na wafanyakazi hao baada ya taratibu za kuwalipa mafao yao kukamilika.

“Taarifa nilizonazo ni kwamba kuna yadi ya kampuni iko huko Dar es Salaam; mipango ya kuiuza yadi hiyo inaendelea na kiasi cha fedha kitakachopatikana kitasaidia kumaliza tatizo hilo,” alisema.

Kuhusu michango ya wafanyakazi hao kutowasilishwa PPF, Lukule alisema mwenye majibu ni mkurugenzi wao na akasema hata yeye michango yake haiwasilishwi.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia madai ya wafanyakazi hao ambao pia bila kufafanua walimtuhumu kuipoteza serikali mapato yake halali, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Johnson alisema madai hao hayana ukweli kwani ameendelea kuwalipa wafanyakazi hao mishahara yao ya kila mwezi pamoja na kwamba hawana kazi ya kufanya.


Alipoulizwa lini ilikuwa mara yake ya mwisho kuwasilisha michango ya wafanyakazi hao PPF, alikata simu baada ya kudai hana muda wa kupoteza wa kuongea na waandishi wa habari. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment