Tuesday, 9 September 2014

UCHAGUZI MKUU WA 2015 WAMUWEKA ZITTO KABWE NJIAPANDA

Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe anaonekana yuko njiapanda kati ya nia yake ya kugombea urais au ubunge, lakini kwa jinsi mwenendo wa kuandika Katiba Mpya ulivyo, ni dhahiri ataendelea kugombea nafasi kuingia bungeni.

Hata hivyo, mbunge huyo kijana hatarudi Kigoma Kaskazini ambako ameongoza kwa vipindi viwili; atagombea jimbo la Kigoma Mjini.

Septemba 23 mwaka huu, Zitto atakuwa akitimiza umri wa miaka 38, lakini Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, ambayo hakuna shaka kuwa ndiyo itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani, inaruhusu mgombea mwenye miaka kuanzia 40, umri ambao Zitto hatakuwa ameufikia mwakani atakapokuwa na miaka 39.

“Kama Katiba haitaniruhusu nitafanya kitu ambacho kitanifanya niendelee kufanya siasa na possibly (uwezekano ni kwamba) ninaweza kugombea ubunge Jimbo la Kigoma mjini,” alisema Zitto katika mahojiano na Mwananchi wiki iliyopita.

“Suala la umri wa urais limekuwa likihusishwa sana na Zitto, hii siyo sahihi. Hili suala lipo katika Rasimu ya (Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph) Warioba. Wengine hawataki suala hili libadilishwe ili tu nisipate nafasi, lakini ukweli ni kwamba zaidi ya nusu yaani asilimia 53 walipendekeza umri wa kugombea urais upugunguzwe… siyo mimi ni wananchi.

“Tuangalie nchi zinazotuzunguka kiwango cha umri wa kugombea Urais, Kenya umri ni miaka 35, Uganda miaka 35, Rwanda, Burundi, Senegal, Mozambique, Zimbabwe ni miaka 35. Uingereza wao hawana hata umri. Mtu yoyote anayegombea ubunge anaweza kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza,” alisema.

Zitto alionya kuwa ujana siyo sifa pekee ya kuutaka urais. Anaona zipo nyingine za kikatiba, kihaiba na za kijamii.

“Kama mna sifa mmezipanga, zote zipo pale. Sasa kama kuna kijana mwenye sifa, kwa nini azuiwe?” anahoji kwa ukali kidogo.

Hata hivyo, Zitto bado ana nia ya kushika nafasi hiyo ya juu nchini, akisema haoni mtu mwenye sifa zaidi yake.

Zitto alisema nia yake ya kugombea urais ni kutaka kukamilisha ndoto yake ambayo ni kuona kila Mtanzania anafaidika na rasimali zilizopo.

“Simwoni mwingine anayeweza kuiongoza nchi hii kwa sasa zaidi yangu. Nchi hii kwa sasa inahitaji mtu mwajibikaji hata kama jambo hilo litamletea madhara, mwenye uadilifu usio na shaka, anayeyajua matatizo ya wananchi na awe na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania,” alisema Zitto.

”Sina shaka na uwezo wangu na uzalengo wangu. Mfano nilipotoa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu watu waliamini ni Chadema tu ndiyo watakaotia saini zao, lakini wapinzani wote walisaini na watano kutoka chama tawala.”

Mapema mwaka huu, Zitto alivuliwa nyadhifa zake zote Chadema na mustakabali wake kwa sasa unasubiri uamuzi wa mahakama, hali ambayo inafanya uwezekano wa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho kuwa mgumu.

Lakini hilo si tatizo kwake.
“Nategemea kuendelea kuifanya kazi ya siasa. Nitakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa, lakini siyo CCM,” alisema Zitto alipoulizwa atagombea urais kwa chama gani kutokana na hali kuwa tete kwake ndani ya Chadema.

Licha ya tuhuma nyingi kwamba alikuwa mbioni kujiunga na CCM, Zitto alisema hawezi kujiunga na chama hicho tawala kwa kuwa ndoto yake ni kuona demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini inakua kwa kuuimarisha upinzani.

Alisisitiza kuwa ndoto yake ni kuona Tanzania ikiongozwa na Rais kutoka upinzani.

“Kama nikikosa nafasi ya kuwania urais, nitawapima waliopo na nitamfanyia kampeni ninayeona anafaa. Ninapenda kuona mgombea wa upinzani anashinda,” alisema Zitto.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment