Friday, 19 September 2014

TACELAM WASEMA LUGHA YA KUFUNDISHIA KIKWAZO CHA MAENDELEO YA ELIMU NCHINI

Dk Newton Kyando na Chelestino Mofuga
BARAZA la Uongozi wa elimu, Utawala na Usimamizi (TACELAM) limesema matumizi ya lugha ya kufundishia ni moja ya tatizo linalozorotesha maendeleo ya elimu nchini.

Wakizungumza na wanahabari hivikaribuni, viongozi wa baraza hilo lenye makao yake makuu mjini Iringa wamesema ipo haja kwa wadau wa sekta hiyo wakakubaliana ni lugha ipi kati ya kingereza au Kiswahili iwe ya kufundishia toka chekechea hadi chuo kikuu.

“Kuna shida katika mfumo wetu, mtoto anafundishwa kwa lugha ya Kiswahili chekecheka hadi darasa la saba na baada ya hapo lugha inabadilika, masomo mengi anasoma kwa kingereza,” alisema Mwenyekiti wa TACELAM, Chelestino Mofuga.

Mofuga alisema hali hiyo imewafanya wanafunzi wengi wajikute katika mazingira ya kushindwa kumudu lugha ya kingereza hata wanapohitimu mafunzo ya vyuo vikuu.

“Ni muhimu tukaangalia suala hili kwa kina, kama ni Kiswahili basi kitumike toka shule ya msingi hadi chuo kikuu na kama ni kingereza iwe hivyo hivyo,” alisema.

Katibu wa TACELAM, Dk Newton Kyando alisema; “mfumo wa matumizi ya lugha zote mbili unawaweka wasomi wengi njia panda ya kushindwa kuyafafanua mambo kwa lugha tofauti na ile waliyomalizia.”

Akitoa mfano, Dk Kyando alisema; “Profesa wa kemia anaacha matumizi ya Kiswahili katika somo hilo baada ya kuingia kidato cha kwanza  jambo linalompa shida ya kufafanua mambo mbalimbali kuhusu somo hilo kwa lugha ya Kiswahili.”

Wakati huo huo alisema, Profesa wa Kiswahili sio rahisi sana kwake kufafanua mambo kwa lugha ya kingereza kama atakavyofanya kwa lugha aliyobobea kwahiyo ni muhimu watanzania wakakubaliana lugha moja ya kufundishia toka ngazi ya chini hadi chuo kikuu.

Alisema kwa kawaida binadamu anakuwa katika mazingira mazuri ya kufundishika na kuyafahamu mambo anapokuwa na umri mdogo kwahiyo ni muhimu kama lugha ya kufundishia ni Kiswahili au kingereza basi ikawa hivyo toka ngazi ya chini.

Alisema kuporomoka kwa elimu kumelifikisha taifa mahali ambapo mtu mwenye elimu chini ya chuo kikuu anafanya kazi vizuri zaidi kuliko yule aliyemaliza chuo kikuu.

“Kwa mfano angalia katika sekta ya umeme, mwanafunzi aliyemaliza VETA anaweza kufanya kazi nzuri zaidi kuliko yule aliyemaliza fani hiyo chuo kikuu na wakati mwingine sio jambo la ajabu kuona aliyemaliza chuo kikuu anamwajiri wa VETA ili amfanyie kazi ambayo naye kasomea,” alisema.

Novemba 4-6, baraza hilo linatarajia kuendesha kongamano la kimataifa linalolenga kuwajengea uwezo watoto katika ushiriki wa masuala ya sayansi na teknolojia.


Kongamano hilo linalotarajia kushirikisha wageni zaidi ya 100 kutoka mataifa mbalimbali duniani litafanyika Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment