Monday, 1 September 2014

REST IN PEACE DAUDI MWANGOSI, YALIKUWA MASAA, SIKU, MIEZI SASA UMETIMIZA MIAKA MIWILI TANGU UTUTOKE KWA KIFO CHA KINYAMA

Moja ya Sifa kubwa aliyokuwa nayo Daudi Mwangosi (mwanzoni pichani) ambayo huenda wanahabari wengi hawana ni usikivu. Alikuwa ni mtu wa kupenda kujifunza kila siku.
Aliyevaa miwani ni mtuhumiwa wa mauaji ya Daudi Mwangosi, Pasificus Cleophace Simon akifikishwa mahakamani hivikaribuni
Ataendelea kukumbukwa kwa usikivu wake. Hapa ilikuwa siku chache kabla ya kifo chake akiwa kazini huko wilayani Kilolo
.
Aliuawa mbele ya macho ya mkuu huyu wa Polisi, Michael Kamuhanda, wakati huo akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa

ZILIKUWA saa, siku, wiki, mwezi, miezi, mwaka na sasa ni miaka miwili tangu mpiganaji Daudi Mwangosi aiage dunia mbele ya wanahabari wenzake huko kijijini Nyololo Wilayani Mufindi.

Ilikuwa Septemba 2, 2012 mchana, Mtuhumiwa wa mauaji hayo, Pacificius Cleophace Simoni alipomlipulia bomu Daudi Mwangosi na kusababisha kifo chake.

Kwa kukusudia Simoni amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumuua Mwangosi kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura ya 16 .

Marehemu alikuwa Nyololo kwa ajili ya kuripoti na kutoa taarifa kwa umma juu ya mkutano uliokuwa ufanywe na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

KESHO Septemba 2, itaendelea kuwa siku ya kumbukumbu muhimu kwa wanahabari wote nchini kutokana na tukio la kinyama lililofanywa kwa mwandishi mwenzetu.

Kifo chake kimeacha majonzi makubwa si tu kwa ndugu na wanafamilia lakini wanahabari na Taifa kwa ujumla.

Kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya tasnia ya habari, tutaendelea kumkumbuka na kuuthamini kwa hali na mali mchango wake kwa taifa hili.

Tunaahidi kuendelea kuyaenzi yale yote mazuri aliyoanza na kuyadhamiria. Mwangosi alikuwa mtu mwenye staha, mvumilivu, mpole, msikuvu na asiyependa kuona haki ya mtu inapotea kionevu.

Ameonyesha hayo ndani na nje ya tasnia ya habari. Ushujaa wake katika kufuatilia mambo yenye maslai ya umma lakini yanayotaka kufichwa na watawala ulimjengea heshima kubwa kwa umma.

Mwangosi ameondoka lakini ametuachia kitu nyuma yake. hicho si kingine zaidi ya kuwa SAUTI za WASIOSIKIKA. 

Sehemu yetu kubwa tunasaliti wajibu huo. Tumekuwa SAUTI za mabwanyenye, sauti za wanaofisadi nchi, sauti za wanaonyima uhuru na haki za watu wengine, sauti za wazushi, waongo, wenye fitina, sauti za wanaojifanya wako kwa maslai ya watu kumbe kwa maslai yao na sauti za wasiotaka sauti za WASIOSIKIKA zisikike.

Tunapo mkumbuka Mwangosi tukumbuke pia kwamba tunayo nafasi ya kubadili mitizamo na fikra zetu ili wote bila kujali itikadi wala dini tufaidi kwa pamoja rasilimali za nchi hii.

Tuna wajibu wa kufichua yanayoendelea kufichwa ndani na nje ya vyama vya siasa, ndani na nje ya taasisi za umma, ndani na nje ya serikali, ndani na nje ya makundi mbalimbali ya kijamii na maendeleo.

Tunapofanya hivyo ni muhimu tukazingatia misingi ya taaluma hii kama hatua ya kulinda heshima ya kuwa mhimili wa nne wa dola ambaye kazi yake kuu ni kuwa msemaji wa wasio na sauti.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.

RIP Daudi Mwangosi

Reactions:

0 comments:

Post a Comment