Wednesday, 3 September 2014

NURU HEPAUTWA ATUNISHA MFUKO WA OVERCOMERS REDIO, ACHANGIA SH MILIONI 4

Nuru Hepautwa (kushoto) akimkabidhi Askofu Boaz Sollo Sh 500,000 zikiwa ni sehemu ya mchango wake wa Sh Milioni 4 kwa redio Overcomers FM ya mjini Iringa
Cheers 
Na keki ikaliwa katika hafla hiyo ya miaka minne ta redio Overcomers FM
Askofu naye akitanua mdomo ili keki iingie vizuri kinywani mwake
Katika sherehe hiyo waliokuwepo wadau mbalimbali wakiwemo alemavu
wageni waalikwa
KADA maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mjini Iringa, Nuru Hepautwa ametoa Sh Milioni 4 kama mchango wake kwa redio ya dini ya mjini Iringa, Overcomers FM.

Hepautwa ambaye pia ni mfadhili wa mashindano ya soka yaliyojizolea umaarufu mjini Iringa ya Hepautwa Cup alitoa mchango huo juzi wakati redio hiyo ikiazimisha miaka minne tangu ianze kurusha matangazo yake hewani.

Awali meneja wa redio hiyo, Elinami Kyungai alisema ili kuongeza ufanisi wameanza kujenga studio zao katika eneo la Zizi la Ng’ombe mjini hapa ili zitakapokamilika waondoke katika jengo la kupanga wanalotumia sasa.

Kyungai alisema ili kukamilisha ujenzi wa studio hizo ambao umefikia hatu za kati wanahitaji zaidi ya Sh Milioni 120.

“Tukiwa katika hekaheka za kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa studio zetu, tuko pia katika mpango wa kutanua masafa ili tusikike kaika mikoa mingi zaidi,” alisema.

Alisema kwasasa redio yao inasikika katika wilaya zote za mkoa wa Iringa na mpango wao ni kurusha matangazo yao katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

Akichangia harakati za redio hiyo, Hepautwa aliipongeza redio hiyo kwa
mafanikio makubwa inayoendelea kupata wakati ikitekeleza wajibu wake wa kuhabarisha umma taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo ya manispaa ya Iringa, mkoa wa Iringa, Taifa na duniani kwa ujumla.

“Kazi inayofanywa na redio hii na vyombo vingine vya habari hakuna ubishi kwamba vinaifanya tasnia ya habari iheshimike kama muhimili wa nne wa dola” alisema.

Alisema moja ya vipimo vya dalili za demokrasia katika jamii ni kuwapo kwa vyombo vya habari vilivyo huru.

“Katika kila taifa lenye demokrasia, wananchi wake wanapaswa kuwa na fursa ya kujadili masuala yao kwa uhuru na amani. Huo ndio mfumo wa kweli wa demokrasia na hauwezi kuwapo bila kuwa na uhuru wa habari ambao ndio unaoweza kuiendeleza” alisema.

Alisema zaidi ya miaka 60 baada ya Azimio la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu kutangaza haki ya kila mtu “kutafuta, kupokea na kutoa taarifa na mawazo kupitia chombo chochote cha habari bila vikwazo vyovyote,” watanzania wanashuhudia jinsi haki hiyo inavyoendelea kukua kwa kasi kubwa nchini na ushahidi ni ongezeko kubwa la vyombo vya habari hapa nchini.

Hepautwa alisema miaka kumi iliyopita hapa Iringa kulikuwa na chombo kimoja tu cha habari, Redio Country FM, lakini kwa jinsi serikali inavyojitahidi kuheshimu misingi ya azimio hilo, vyombo vya habari hapa hapa Iringa vimeongezeka kutoka kimoja hadi zaidi ya 13.


Mbali na Redio Overcormers ambayo hii leo inatimiza miaka minne, vyombo vingine vya mjini hapa ni pamoja na Ebony FM, Nuru FM, Furaha FM, Hope FM, Kwanza Jamii Redio, Kwanza Jamii Gazeti, Daraja Letu gazeti, Furaha Gazeti, Jarida la Mkombozi na blogs mbalimbali ikiwemo ile inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa ya www.frankleonard.blogspot.com ambayo ni maarufu kwa jina la BONGO LEAKS.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment