Saturday, 13 September 2014

NI FREEMAN MBOWE PEKEE KINYANG'ANYIRO CHA MWENYEKITI CHADEMA TAIFA


Hamkani hali si shwari ndani ya Chadema! Kansa Mohamed Mbaruku, Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Mkoa wa Tabora, amejitoa kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa, hivyo kumfanya kwa mara nyingine Freeman Mbowe kuwa katika mashindano ya 'farasi' mmoja.

Kwa mujibu wa 'Mwananchi Breaking News', Mbaruku ameamua kujitoa kwa madai kwamba katiba ya chama hicho imekiukwa na akasema atakwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga uchaguzi huo na kuomba ufafanuzi wa kikomo cha uongozi.

Mbaruku amejitoa siku moja tu baada kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake, ambao umepangwa kufanyika kesho Jumapili Septemba 14.

Hata hivyo, wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kwamba kujitoa kwa mgombea huyo kunaweza kusababisha mpasuko ndani ya Chadema kutokana na malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi ya uongozi kwamba unaendesha chama kama 'taasisi binafsi'.

Awali Mbaruku aliwasilisha pingamizi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, ambapo pamoja na mambo mengine, alidai kwamba Mbowe hana sifa kikatiba ya kugombea tena nafasi hiyo.

Pia duru za siasa ndani ya chama hicho zilieleza kwamba, majina mawili yaliyotangazwa na Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda katika chama hicho, Benson Kigaila, kwamba nao walijitokeza kugombea nafasi ya uenyekiti, Daniel Ruvanga na Garambenela Frank, yalikuwa majina hewa yaliyolenga kumsafishia njia Mbowe ya kubakia kuwa mgombea pekee baada ya kuenguliwa kwa Mbarouk.

Inaelezwa kwamba, Katiba ya Chadema hairuhusu kiongozi wa nafasi hiyo kugombea vipindi zaidi ya viwili vya miaka mitano.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment