Wednesday, 10 September 2014

NDOTO ZA DK KIGWANGALLA KUWA RAIS WA TANZANIA ZEYEYUSHWA BAADA YA MAKUBALIANO YA RAIS KIKWETE NA TCD

Dk Hamis Kigwangalla
MAAZIMIO yaliyofikiwa katika kikao cha Vyama vya Siasa vyenye wabunge vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete juzi, yamemaliza ndoto za Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Dk Kigwangalla alitangaza nia ya kuwania nafasi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam siku tatu zilizopita.

Ndoto za Dk Kigwangalla aliyezaliwa Agosti 7, 1975 zitakuwa zimeyeyuka baada ya TCD na Rais Kikwete kukubaliana kusitisha mchakato wa kupata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Badala yake viongozi hao  wamekubaliana Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ipelekewe bungeni kufanyiwa marekebisho ili iendelee kutumika katika  Uchaguzi Mkuu  wa mwakani.

Mambo ambayo vyama hivyo vimekubaliana ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, mshindi wa uchaguzi wa Rais apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, matokeo ya rais yaruhusiwe kupingwa mahakamani na kuruhusu mgombea binafsi.

Kwa makubaliano hayo sifa za mgombea nafasi hiyo ya nchi kwa mujibu wa Katiba zinabaki zile zile ikiwemo ya umri wa miaka 41 inayomuondoa Dk Kigwangalla katika kinyang’anyiro hicho.

Kwasasa Dk Kigwangalla ana miaka 39 na itakapofika Agosti 7, mwakani atakuwa na miaka 40 itakayomuondolea sifa inayotakiwa ya miaka 41 ili aweze kuwania nafasi hiyo.

Kama sifa hiyo haitarekebishwa tumtakie heri, Dk Kigwangalla kwenye harakati zingine za kisiasa ikiwemo ya kuwania ubunge katika jimbo lake za Nzega..

Kuyeyuka kwa ndoto za Dk Kigwangalla kunamuacha kijana mmoja, Naibu Waziri wa Mawasliano Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba katika kinyanga’anyiro hicho.

Makamba alitangaza nia ya kuitaka nafasi hiyo ya juu kabisa ya utawala hivikaribuni.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment