Thursday, 11 September 2014

MUFINDI WASEMA VITI MAALUMU UBUNGE SASA ZAMU YAO, NI AMA LEDIANA MNG'ONG'O AU RITTA KABATI AACHIE NGAZI

Ritta Kabati na Lediana Mng'ong'o
Baadhi ya wajumbe wa UWT, Mufindi katika kikao chao cha hivikaribuni
VITA kali ya kisiasa katika kinyang’anyiro cha kuwapata wabunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa inatarajiwa kushuhudiwa katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwakani baada ya baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi kuweka wazi kwamba mwaka ujao ni zamu yao.

“Ni zamu yetu, lazima nao wakubali kwamba ni zamu yetu, maana tangu mwaka 2000 nafasi ya viti maalumu wamekuwa wakipata wenzetu wa Iringa. Muda umefika nao watuunge mkono kabla hatujapata katiba Mpya,” alisema mmoja wao ambaye hata hivyo hakutaka kutaja jina.

Tamko la akinamama hao wa wilaya ya Mufindi linawaweka katika hatari ya kutorudi bungeni, Ritta Kabati na Lediana Mng’ng’o ambao wote ni wabunge wa viti maalumu kupitia mkoa huu wa Iringa.

Wakati Lediana Mng’ong’o  amekuwa mbunge wa viti maalumu kupitia CCM tangu kwa awamu ya tatu sasa tangu mwaka 2000, Ritta Kabati anakaribia kumaliza awamua yake ya kwanza ya miaka mitano.

“Ndio mwaka 2015, Mng’ong’o atakuwa anatimiza miaka 15 tangu achaguliwe kwa mara ya kwanza mwaka 2000 kuwa mbunge wa viti maalumu. Na huyu Ritta Kabati atakuwa anamaliza miaka yake mitano tangu aingie katika kiti hicho mwaka 2010,” alisema mwingine.

Alisema kama sio wote wawili basi mmoja wao ni lazima aondoke kupisha mama kutoka wilaya ya Mufindi kuchukua nafasi mojawapo.

“Uongozi ni kupokezana vijiti, haiwezekani ikawa Iringa tuu  kila mwaka, huo ni uwakilishi wa aina gani?.....ni muhimu nao wakaliona hilo na kuisaidia Mufindi kupata mwakilishi bora,” alisema.

Wakati Lediana Mng’ong’o amekuwa kimya sana kisiasa tofauti na awamu zake mbili zilizopita hali inayowafanya baadhi ya wanaCCM wamzushie kwamba hagombei tena viti hivyo, Ritta kabati amekunuliwa akikosoa utaratibu wa sasa wa kupata wabunge wa viti maalumu.

 “Moja ya jambo ninalounga mkono katika mchakato huu wa kupata Katiba Mpya ni kufuta utaratibu unaotumika sasa wa kupata viti maalumu vya wanawake.”

 “Siku hizi wabunge wanawake wa viti maalumu tunaitwa wabunge wa vitanda maalumu, huu ni udhalilishaji kwasababu wengi wanahisi hatuwezi kupata ubunge kwa kupigiwa kura na wananchi,” alisema.

Alisema utaratibu unaotumiwa na nchi kama Uganda na Rwanda kupata wawakilishi wanawake katika mabunge yao ndio unaopaswa kutumiwa na Tanzania na kama ikishindikana basi wanawake nao wapewe nafasi sawa na wanaume ya kugombea moja kwa moja kwenye majimbo ya uchaguzi.

“Tumetembelea Uganda na Rwanda, kule hawaiti viti maalumu vya wanawake, wanaita viti vya wilaya vinavyoshindanisha wanawake wa vyama mbalimbali katika wilaya hizo,” alisema.

Tuendelee kusubiri, wakati Uchaguzi Mkuu ukikaribia tutasikia na kushuhudia mengi toka kwa wanasiasa

Itaendelea……………………………………

Reactions:

0 comments:

Post a Comment