Monday, 8 September 2014

MNEC AGAWA BAISKELI KWA VIONGOZI WA CCM WA KATA ZOTE ZA WILAYA YA MUFINDI

Mmoja kati ya makatibu wa UWT wa kata za wilaya ya Mufindi akipokea toka kwa naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa msaada wa baiskeli zilizotolewa na Mwenyekiti na MNEC wa wilaya hiyo Marcelina Mkini (kushoto) anayecheka nyuma ni Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu
Akitoa maelekezo ya jinsi baiskeli hizo zinavyotakiwa kutumika
Sehemu ya wajumbe wa baraza kuu la UWT wilaya ya Mufindi katika kikao chao cha hivikaribuni
wajumbe wengine

Mgimwa na Mkini wakiwaongoza wajumbe wa Baraza Kuu la UWT kucheza nyimbo mbalimbali zinazoisifu CCM
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anayewakilisha wilaya ya Mufindi, Marcelina Mkini ametoa msaada wa baiskeli 60 zitakazorahisha utendaji kazi wa viongozi wa chama hicho ngazi ya kata.

Watakaonufaika na msaada huo ni makatibu kata wa kata zote 30 za wilaya hiyo na makatibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa kata hizo.

Wakati makatibu kata walikabidhiwa baiskeli zao mwishoni mwa mwezi uliopita katika hafla iliyohudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Jenister Mhagama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wale wa UWT walikabidhiwa baiskeli zao juzi na naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa.

Akikabidhi baiskeli hizo Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini alisema wanawake wamendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya chama hicho hivyo ni muhimu wakaendelea kupewa misaada wanayohitaji.

“Wanawake wapo katika kundi lisiloteteleka kisiasa. Mkisema hamrudi nyuma kwahiyo nipo tayari kuyafanyia kazi yote mtakayonishauri kwa ajili ya maendeleo ya chama chetu,” alisema.

Alisema kundi lingine ambalo ni muhimu sana kwa maendeleo ya chama hicho ni wazee ambao sio rahisi kuwabadilisha kutoka katika imani wanazoziamini.

“Lakini kundi la tatu ni la vigeugeu, hili ni la vijana, leo wakisema hili kesho wanaweza kusema lingine kwahiyo akina mama mnatakiwa kukisaidia chama kulielimisha kundi hili,” alisema huku akimpongeza Mkini kwa msaada mkubwa alioutoa kwa UWT.

Akizungumzia sababu za kutoa msaada huo, Mkini ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT wa wilaya hiyo alisema katika ziara yake aliyofanya hivikaribuni katika kata zote za wilaya hiyo aliguswa na mchango wa viongozi hao katika kukijenga chama na changamoto hasa ya usafiri wanayopata wanapotaka kutembelea tawi moja hadi lingine.

“Tumeanza na baiskeli, tunaomba Mungu atusaidie ili tuboreshe zaidi vyombo hivi vya usafiri, ikiwezekana makatibu wetu hawa wapate pikipiki,” alisema.

Katika ujumbe wake kwa wajumbe wa baraza hilo la UWT, Mkini alisihi wanawake hao kuwapuuza wanawake wanaojipitisha katika majimbo ya uchaguzi wilayani humo kwa lengo la kujitengnenezea mazingira ya kukubalika wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.

“Muda bado haujafika, tuwaache wabunge wetu wafanye kazi, subirini muda ufike ndio muingie, mkiwapokea wanaojipitisha sasa mnawapa kiwewe wabunge walioko madarakani na badala ya kushughulikia maendeleo yenu, wanajikuta wanashughulika na wanayosikia” alisema.

Katika kikao hicho Katibu wa CCM wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu alitoa mada tatu kuhusu umuhimu wa jumuiya katika shughuli za chama, vikao vya chama na mambo ya kuzingatai na maandalizi ya uchaguzi, uenezi wa chama na mawasiliano.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment