Saturday, 20 September 2014

MKURUGENZI WA TIGO AFAGILIWA IRINGA VIJIJINI

Mkurugenzi wa Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya Tigo, Jackson Kiswaga akipongezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa (mwenye kofia) kwa mchango wake mkubwa wa maendeleo wilayani humo
MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Steven Mhapa amempongeza Mkurugenzi wa Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya Tigo, Jackson Kiswaga akisema ni mdau wa kweli wa maendeleo wa wilaya hiyo.

“Tuliomba wengi lakini katika hao wengi wewe hukusita kutusaidia, tunaamini umeguswa na kero yetu. Tunakupongeza sana na tutaendelea kukupa ushirikiano. Haya ndio maendeleo,” alisema wakati Kiswaga akikabidhi msaada wa pikipiki iliyoombwa na Jumuiya ya Watumiaji Maji Kata ya Nzihi, Iringa vijijini.

Mhapa alimuomba Kiswaga asikatishwe moyo na baadhi ya watu wasioitakia mema wilaya ya Iringa na wale wanaohusisha na harakati za siasa kila jambo la maendeleo linalofanywa na wadau wa maendeleo.

Kiswaga mwenyewe akasema; “ninapopata nafasi ya kushirikiana na wenzangu katika maendeleo yetu, sitaacha kutoa mchango wangu, nimefanya hivyo muda mrefu uliopita, nafanya hivi sasa na nitaendelea kwa siku nyingi zijazo.”

“Naomba Mungu aendelee kunijalia afya njema kama alivyomjalia umri mrefu mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Marehemu John RockeFeller pamoja na kusumbuliwa maradhi yaliyodhaniwa yangemaliza uhai wake katika umri wake wa miaka 50,” alisema.

Taarifa zinaonesha kabla na baada ya kufariki familia ya Rockefeller imeendelea kufanya biashara kubwa za mafuta, majengo na ndio wamiliki wa baadhi ya vyuo maarufu huko nchini Marekani kikiwemo chuo cha Havard na Stanfod kupitia Rockefeller Foundation.

Katika uhai wake wa miaka 98, John Rockefeller alidhaniwa angekufa akiwa katika umri wa miaka 50 baada ya kuugua maradhi ya tumbo na mengine ya kimwili yaliyopelekea apoteze nywele zake zote za mwili.

Ilipofika mwaka 1901, John Rockfeller hakuwa na nywele yoyote mwilini mwaka na akaanza kuvaa nywele za bandia kichwani ili kuficha hali aliyokuwa nayo.

Akiwa amepoteza matumaini ya kuendelea kuishi, Rockfellaer alianza kugawa sehemu ya utajili wake kwa masikini na kuanzisha taasisi mbalimbali zinazoendelea kutoa huduma za afya na elimu nchini humo.

Pamoja na hofu aliyokuwa nayo, kutoa kwake kwa lengo la kusaidia wasiojiweza, kwa mujibu wa Kiswaga ndiko kulikomfanya asifariki akiwa katika hali tete wakati ana umri wa miaka 50 na badala yake akafa akiwa kikongwe akiwa na miaka 98.

“Najitahidi kufanya kama John Rockefeller, nimesaidia huko nyuma, nasaidia sasa na nitaendelea kusaidia kwa kadri napopata fursa na ziada. Naamini nikifanya hivyo maombi ya kunitakia afya njema yatakuwa mengi na hivyo nitakuwa nanyi kwa miaka mingi,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nzihi, Lazaro Kindole alisema Kiswaga ni mtendaji wa kweli kwani akiahidi jambo ni lazima atekeleze tena kwa muda mfupi.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Magubike, Lenatha Mbilinyi alisema; “Kiswaga anajitambua na ndio maana siku zote yupo jirani na watu na mpenda maendeleo, tuendelee kumlea.”

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nzihi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidamali, Daima Luvanda alisema; “Kiswaga ni mtu wa aina yake. Anasaidia mengi hivyo ni muhimu akaungwa mkono.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment