Thursday, 4 September 2014

MKURUGENZI WA NHC AWAASA VIJANA MAISHA BORA HAYAJI KWA KUKAA VIJIWENI NA KUILAMU SERIKALI

Mkurugenzi wa NHC, Nehemia Mchechu
wahitimu wa chuo cha sayansi ya afya Bulongwa


Mzee Butinini alikuwepo kushuhudia mjukuu wake akihitimu
MKURUGENZI wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Nehemia Mchechu amewataka vijana kuachana tabia ya kukaa vijiweni na kuitolea serikali lawama zisizo na msingi na badala yake watumie fursa zinazowazunguka kujiajiri.

Aliyasema hayo hivikaribuni kwenye mahafali ya nane ya Chuo cha Sayansi ya Afya kilichopo Bulongwa wilayani Makete mkoani Njombe. Chuo hicho kinamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Msechu alisema wanaotafuta njia ya mkato kufikia ndoto zao za mafanikio uishia kulalamika kwa kukosa kile wanachotaka tofauti na wale wanaohangaika kujiendeleza kimasiaha kwa njia halali na kwa nidhamu.

Alisema taasisi mbalimbali zinaweza kujitokeza na kusaidia katika shughuli za uwekezaji kama wana Makete watashirikiana na serikali yao kuzitangaza fursa walizonazo na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

“Maisha bora ya mtu hujengwa na mtu mwenyewe kwa kujituma katika kujiletea maendeleo, ukiwa usingizini hakuna mtu atayekuja kukuzindua, kwahiyo ni muhimu ukazinduka wewe mwenyewe kutokana na hali hali ya maisha ya sasa,” alisema.

Awali Askofu Msaidizi wa KKKT Dayosisi ya Kusini na Kati, Filimoni Kauka aliwakumbusha wahitimu hao kuzingatia maadili ya kazi yao na kuepuka vishawishi katika utoaji wa huduma.

“Kama viapo mnavyoapa wakati mnapomaliza masomo yenu na mnapoanza kazi, tumieni viapo hivyo kama muongozo wenu wa kutoa na kuboresha huduma ya afya katika jamii,” alisema.


Askofu Kauka alisema utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa ni jambo nyeti linalopaswa kufanywa kwa kuzingatia msingi wa maadili na weledi hali itakayosaidia kumaliza kasoro na changamoto zilizopo hivi sasa katika utoaji wa huduma za afya.

Alisema zipo taarifa za uwepo wa baadhi ya wauguzi wanaofanya kazi bila ya kuzingatia maadili ya kazi zao hali inayosababisha wanaohitaji huduma kujikuta katika mazingira ya kupata matatizo zaidi ya yale yaliyowapeleka hospitalini.

Amewataka watoa huduma hao kuachana na tabia ya kupenda rushwa kwani ushahidi uliopo katika maeneo mengi unaonesha vitendo hivyo vimekuwa vikichelewesha upatikanaji wa huduma hata kama zipo.

Naye makamu mkuu wa Chuo hicho, John Matara alisema mbali na mafanikio kiliyoyapata chuo hicho bado kinakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa vifaa vya kufundishia pamoja na walimu

Matara ameomboa serekali na wadau wa sekta ya afya kunusuru hali hiyo kwa kuchangia michango mbalimbali itakayosaidia ujenzi wa majengo ya kisasa yanayoendana na hadhi ya elimu itolewayo katika  chuo hicho .

Reactions:

0 comments:

Post a Comment