Wednesday, 17 September 2014

MHANDISI MNANDI MRUTU ACHANGIA SH MILIONI 3 UJENZI WA MAABARA SEKONDARI YA KIRONGAYA

Mhandisi Mnandi Mrutu akitoa zawadi kwa mmoja wa wahitimu wa shule hiyo

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakifuatilia shughuli zilizokuwa zikiendelea wakati wa mahafali ya shule hiyo
MDAU wa Maendeleo ya Elimu nchini, Mhandisi Mnandi Mrutu ameahidi kutoa Sh Milioni 3 ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari ya Kirongaya ya wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Alitoa ahadi hiyo kwenye mahafali ya 24 ya kidato cha nne yaliyokwenda sambamba na harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa na maabara unaoendelea shuleni hapo.

Mkuu wa shule hiyo, Gabriel Kitururu alisema katika harambee hiyo iliyowezesha jumla ya Sh Milioni 5,343,450 kupatikana hadi kukamilika kwake maabara hiyo inahitaji zaidi ya Sh Milioni 76.

Akizungumzia maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo, Mrutu alisema; “yataletwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na wadau wao wa maendeleo akiwemo mdau mkuu ambaye ni serikali.”

Aliwasihi wananchi wa wilaya hiyo kuhamasishana kwa nguvu zao zote kuchangia shughuli za maendeleo zenye tija ya jumla kwa kizazi kilichopo na kijacho badala ya sherehe za kupita.

“Katika maeneo mengi nchini wananchi wengi wamekuwa wakinung’unikia michango wanayoombwa kwa ajili ya maendeleo ya shughuli mbalimbali za maendeleo zinazogusa wengi, lakini wamekuwa wakifurahia kuchangia sherehe kama kitchen party, harusi, vipaimara, ubatizo na zinazofanana na hizo ambazo kimsingi hazina manufaa ya jumla kwa watu wa eneo fulani,” alisema.

Alisema elimu ni urithi wa pekee usioweza kufananishwa na urithi wa mali kwasababu hudumu vichwani mwa wahusika kwa muda wote wa maisha yao.

“Watu wanaweza kurithi nyumba, mifugo, fedha, magari na mali zinginezo, lakini uzoefu unaonesha hivyo vyote kwa mwanadamu ni vitu vya kupita tofauti na elimu ambayo ikishaingia kichwani kwa mtu hudumu kwa maisha yake yote na ndiyo inayoweza kumsaidia kupata mali kwa kadri ya mahitaji yake,” alisema.

Aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwani ni ya manufaa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Kuhusu walimu na ufundishaji, Mhandisi Mrutu amewaasa waalimu kutokatishwa tamaa dhidi ya watoto wasio na uwezo darasani na badala yake watumie mbinu za ziada ili wawafanye wafikie uwezo wa wenzao.

Alisema ni aibu kwa waalimu kukiri ama kuoredhesha watoto wasio na maadili au walioshindwa katika masomo kwani wazazi wanaamini kuwa waalimu wanayo taaluma ya kutosha katika kuleta mabadiliko ya watoto hao.

Akizungumzia changamoto za shule hiyo, Mkuu wa shule hiyo alisema  miundo mbinu mibovu ikiwa ni pamoja na mabweni, madarasa, na vyoo imesababisha idadi ya watoto wanaojiunga katika shule hiyo kongwe kupungua mwaka hadi mwaka.

Sheikh Mkuu wa Kirimanjaro, Shabani Rashid alisema muda umefika kwa wananchi wa wilaya hiyo kushirikiana na wadau wao kurekebisha mazingira ya shule hiyo.

“Kama tunataka kujenga taifa lenye watu wenye uzalendo na taifa lao ni muhimu kwetu sisi kuwa na kitu kitakachowafanya watoto wetu na kizazi kijacho kuiga mazuri tunayofanya vinginevyo uzalendo utapotea na mwishowe kuzorotesha kasi ya maendeleo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment