Tuesday, 9 September 2014

MAMA BAHATI AWAWEZESHA WANAWAKE 10,000 IRINGA KUPATA MIKOPO YA SH BILIONI 5

Mkurugenzi wa Mama Bahati Foundation, Japhet Makau akiteta jambo na mwakilishi wa 5 talents ya Uingereza
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu akikata utepe kuzindua tawi jipya la MBF la wilaya ya Mufindi
Akina mama wakishangilia
Mmoja wa mashuhuda aliyenufaika na mkopo toka MBF akielezea jinsi ulivyomkwamua kiuchumi
Wageni wakifurahi baada ya tawi hilo kufunguliwa
ZAIDI ya Sh Bilioni 5 zimekopeshwa kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 10,000 wa mkoa wa Iringa kupitia taasisi ya Mama Bahati Foundation (MBF) iliyoanzishwa na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Japhet Makau aliyasema hayo wakati MBF yenye makao yake makuu mjini Iringa, ikifungua tawi lake jipya mjini Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Makau alisema mikopo hiyo ya kati ya Sh 750,000 na Sh Milioni 5 imekuwa ikitolewa kwa vikundi vinavyoundwa na wanawake watano watano.

“Shirika linawalenga zaidi wanawake walioko pembezoni; wanawake wanyonge ambao kwa kupitia vikundi vyao vya watano watano, tumekuwa tukiwapa mikopo kwa masharti nafuu,” alisema.

Alisema mikopo hiyo inayotozwa riba ya asilimia 2.5 kwa mwezi ni ya kati ya miezi na mwaka mmoja.

Katika uzinduzi wa tawi hilo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu mbele ya wafadhili wakuu wa MBF, taasisi ya Five Talents ya Uingereza, Mwenyekiti wa Bodi ya MBF, Askofu Mtetemela alisema wazo la kuanzisha taasisi hiyo lilikuja baada ya kuombwa msaada na mama mmoja aisyejiweza zaidi ya miaka mitano iliyopita.

“Baada ya kuniomba nilimuuliza anaitwa nani. Akaniambia anaitwa mama Bahati, nikampa Sh 10,000, nikamshauri aitumie kufanya biashara ya kuuza ndizi mbivu na kumtaka airejeshe baada ya mwezi mmoja,” alisema.

Alisema mama huyo alikuwa mwaminifu kwani baada ya mwezi mmoja alirudisha kiasi hicho cha fedha na ndipo alipoamua kumpa Sh50,000 ili aboreshe biashara yake kwa makubaliano yale yale.

“Baada ya mwezi mmoja mama Bahati alinirejeshea kiasi hicho cha fedha, kitendo hicho kilinidanya niamini watakuwepo wanawake wengi wenye sifa kama ya mama Bahati na ndipo nilipomuomba awatafute wenzake 20 niwasikie matatizo yao na ndipo nilipoamua kuanzisha taasisi hii,” alisema.

Mmoja wa akina mama walionufaika na mikopo ya shirika hilo, Neema Kindole alisema alisema mkopo wa Sh150,000 aliopata kupitia kikundi chao chenye wanachama watano ulimuwezesha kuanzisha biashara ya mgawaha kijijini kwake Sadani.

Alisema biashara hiyo iliendelea kuimarika siku hadi siku na kumuwezesha kuendelea kukopa hadi Sh Milioni moja.

“Kwa faida nayopata na akiba nayojiwekea nifanya mengi ya kila siku kwa familia yangu lakini naloliona kubwa ni baada ya kununua shamba la heka tatu nitakalolitumia kwa kilimo cha umwagiliaji,” alisema na kuongeza kwamba ataliendeleza shamba hilo baada ya kununua mashine ya kumwagilia.

Mkuu wa wilaya ya Mufindi alilipongeza shirika hilo akiahidi kwamba atahakikisha idara ya maendeleo ya jamii ya halmashauri ya wilaya hiyo itaunga mkono jitihada za MBF katika kuwainua wanawake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment