Monday, 8 September 2014

HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA MJINI IRINGA HII LEO BAADA YA DALADALA KUGOMA

Picha na Denis Mlowe
Stendi ya Daladala Miyomboni inavyoonekana baada ya mgomo huo
GARI ndogo za mizigo, baiskeli, pikipiki na bajaj, kwa zaidi ya saa nane hii leo zilitumika kusafirisha abiria katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa baada ya madereva daladala kugoma kutoa huduma hiyo katika tukio ambalo abiria wengine walilazimika kutembea kwa miguu.

Baadhi ya madereva hao walisema mgomo wao ni matokeo ya hasira waliyonayo dhidi ya madereva wa bajaj wanaosafirisha abiria kama daladala hali inayowakosesha mapato.

“Baadhi yao wanapaki katika vituo vinavyotumiwa na daladala, lakini pili, badala ya kusafirisha abiria kama zifanyavyo taxi, yaani ukipata abiria unaondoka, wao wanataka mpaka wachukue abiria wanaoenea katika bajaj zao,” alisema Moses Job.

Job alisema mbali na hilo, nauli zinazotozwa na bajaj hazitofautiani na zile za daladala hali inayofanya abiria wao wakimbilie bajaj kwa kuwa zinajaza mapema, abiria watatu hadi wanne, na kuondoka tofauti na daladala ambayo  kwa wastani inahitaji abiria zaidi ya 10.

Alisema pamoja na kufikisha malalamiko yao kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) wanashangaa hakuna hatu zozote zinazochukuliwa hali inayowaweka katika mazingira magumu kibiashara na kiuchumi.

Akizungumza na madereva bodaboda na bajaj katika kikao kilichofanyika hivikaribuni mjini Iringa, Meneja wa Leseni na Usimamizi wa Barabara, Leo  Ngowi  alisema; “Sisi kama SUMATRA wajibu wetu ni kutekeleza kanuni na sheria zinazosimimia usafirishaji. Hatutakuwa tunatenda haki kama pikipiki au bajaj hizi tutaziruhusu zifanye kazi kila mahali wakati sheria na kanuni zinazuia hilo.”

Ngowi alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo, pikipiki na bajaj zinaruhusiwa kufanya biashara ya usafirishaji katika maeneo ambayo huduma ya usafiri ni ngumu hadi katika vituo vya pembezoni vinavyofikiwa na huduma za usafiri mwingine ukiwemo wa daladala.

“Hatakuwa tunatenda haki kama pikipiki na baja zitapewa leseni za kusafirisha abiria hata katika maeneo yenye huduma za taxi na daladala,” alisema.

Pamoja na madereva hao kuipuuza hoja hiyo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) katika kikao chake na madereva hao aliwataka madereva hao kuzingatia sheria na kanuni za usafirishaji.

Mchungaji Msigwa alisema hayuko tayari kuona haki za watu wengine zinadhulumiwa ili kuwanufaisha watu wengine.
  
“Tunafahamu zipo bodaboda, zipo taxi, zipo daladala na hata maroli. Hawa wote ni watanzania, wote ni lazima wafaidi matunda ya kazi yao, pasiwepo mmoja anayenufaika zaidi,” alisema.

Alisema yeye kama mbunge ni lazima ayazingatie hayo ili kila mtu apate riziki kwa kuzingatia sheria na kanuni zinavyosema.

Kamati ya Usalama Barabarani, haikupatikana kuzungumzia mgomo huo na taarifa zilizoufikia mtandao huu zilidai kwamba walikuwa katika kikao kilichokuwa kinajadili mgomo huo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment