Friday, 5 September 2014

ASKOFU MTETEMELA AKANUSHA MADAI YANAYOMUHUSISHA NA CCM, ATAJA SIFA MBILI ZA RAIS AJAYE

Askofu Donald Mtetemela
ASKOFU Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela amesema yeye sio mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini na kwamba wanaomuhusisha na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwasababu ya msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya wanakosea.

“Niko katika bunge maalumu la katiba nikiwawakilisha waumini wangu, wenye itikadi tofauti. Nikiwa chama fulani sitawatendea haki lakini naitwa CCM kwasababu ya msimamo wangu,” alisema katika mahojiano maalumu na BONGO LEAKS mara baada ya uzinduzi wa ofisi ya asasi ya Mama Bahati Foundation (MBF), mjini Mafinga.

MBF ni taasisi iliyoasisiwa na Mtetemela kwa lengo la kuwainua wanawake wajasiriamali kiuchumi kwa kuwakoposha mikopo ya kati ya Sh 750,000 na ShMilioni Tano kwa kindi cha watu watano.

Askofu Mtetemela alisema anarushiwa madongo hayo na watu waliotaka awe upande wao na asiendelee kushiriki katika bunge hilo ili kuwafurahisha.

“Siwezi kutoka kwasababu ya kuwafurahisha watu fulani. Bunge linaendelea kisheria na akidi ya vikao vyake inaruhusu. Kwanini nitoke?” alisema.

Alisema yeye ni mmoja wa wajumbe wa bunge hilo wanaounda kundi la 201 ambao kimsingi wanawakilisha makundi tofauti ya jamii na sio vyama vya siasa ambavyo tayari vinawawakilishi wake ambao ni wabunge.

Akizungumzia maoni yanayotolewa na baadhi ya taasisi za dini kuhusu kusitishwa kwa mchakato huo  mpaka yatakapopatikana maridhiano ya pande zinazosigana;

Askofu Mtetemela alisema taarifa wanazopata kutoka katika vyanzo visivyo sahihi zimepelekea yatolewe matamko yanayotaka kuhatarisha mchakato huo.

“Kuna mambo yanatokea nje ya bunge na yanaoonekana yana nguvu kwa wananchi lakini ukweli wa mambo huko ndani ya bunge. Tunaijadili rasimu na si vinginevyo, pale tunapoona pako sawa hatuna shida lakini yapo maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa na hiyo ndio kazi tunayofanya kwasababu maana ya bunge maalumu la katiba sio kukubali kila kitu kilicholetwa kwenye rasimu” alisema.

Aliwaomba wajumbe wabunge hilo ambao wamesusia vikao vyake, kurejea ili kwa pamoja wayashughulikie yale wanayotofautiana kwa lengo la kupata maridhiano.

Alisema kinachofanywa na bunge hilo sio hitimisho la watanzania katika kupata katiba mpya na ni makosa kuwahukumu hivisasa kwani baada ya kazi yao, katiba hiyo itapelekwa mbele yao ili ipigiwe kura.

Akizungumzia sifa za Rais ajaye, Askofu Mtetemela alisema kwa mtazamo wake anatakiwa kuwa na sifa kuu mbili bila kujali kama atakuwa kijana au mzee.

“Kwangu mimi umri sio hoja hata kidogo, yoyote anaweza kuwa rais lakini mbali na sifa nyingine zinazotajwa ni lazima awe na sifa kuu mbili kwa mtazamo wangu,” alisema.

Alizitaja sifa hizo kuwa ni lazima awe mwadilifu anayepimika kwa matendo na maneno yake lakini pia ni lazima awe na moyo wa mabadiliko kwa watu wake akiunga mkono juhudi za waliomtangulia katika kuwakwamua watanzania na umasikini.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment