Wednesday, 3 September 2014

AKINA MAMA WENYE VVU IRINGA VIJIJINI WAPEWA MSAADA WA BAISKELI


DC wa Iringa, Dk Leticia Warioba na DED wa Iringa, Pedenciana Kisaka (kulia) wakifurahi wakati Edna Haule anayeishi na maambukizi ya VVU akijaribu kuendesha moja katia baiskeli 50 zilizotolewa kwa vikundi 17 vya akina mama wenye maambukizi hayo

Katika picha ya pamoja
Baadhi ya akinamama wanaounda vikundi hivyo wakishuhudia makabidhiano hayo
Hizi ndio baiskeli zenyewe
SHIRIKA la Utafiti wa Tiba na Afya barani Afrika (AMREF) limetoa msaada wa baiskeli 50 kwa vikundi 17 kati ya 36 vya watoto salama vinavyoundwa na akina mama wenye maaambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) vya Iringa Vijijini.

Akivikabidhi msaada huo katika hafla iliyofanyika katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Iringa, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba aliwapongeza na akawataka wasikate tamaa kwani kuwa na VVU sio mwisho wa maisha.

“Mjisikie wenye amani, majasiri na mnaopaswa kuigwa, kwani wako wengi wana tatizo kama lenu lakini kwasababu ya hofu wanaogopa kupima afya zao na mkiwaona barabarani mnaweza kufikiri wote wana afya njema,” alisema.

Akishukuru kwa msaada huo, mmoja wa akina mama wenye maambukizi hayo, Edna Haule kutoka kijiji cha Migori alisema “tumevunja ukimya tukiamini watanzania wenzetu ambao hawajapima, watajitokeza kujua afya zao ili watakaobainika kuwa na maambukizi waingie kwenye mpango wa mafunzo ya namna ya kutunza afya zao na kutumia dawa.”

Aliwashangaa baadhi ya watanzania wanaoendelea kuwacheka au kuwasimanga wenye maambukizi ya VVU alisema kujua hali ya afya yako kuna faida nyingi ikiwa ni pamoja kukusaidia kujiadhari na maambukizi mapya.

Naye Thadei Madege wa kijiji cha Kihanga alisema baiskeli walizopewa zitawasaidia katika safari zao za kufuata dawa katika vituo vya afya pamoja na kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumzia umuhimu wa vikundi vya watoto salama, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Pudenciana Kisaka alisema vinasaidia kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na inayowasaidia akina mama wenye maambukizi hayo kuzingatia ushauri ili wanapopata mimba wajifungue watoto wasio na maambukizi.

Kisaka alisema kwa kupitia elimu hiyo, vikundi hivyo hufundishwa pia njia zinazosaidia kuwanusuru na maambukizi ya VVU, watoto wanaonyonya kwa akina mama wenye maambukizi hayo.

Mratibu wa Amref anayeshughulikia mradi wa Kutoa Ushauri Nasaha na Upimaji wa VVU, Boniface Magesa alisema baiskeli shirika lao litaendelea kuviwezesha vikundi hivyo kwa kadri litakavyopata nafasi.

“Tumeanza na vikundi hivi, tunajua viko vikundi vingi kwahiyo tunaendelea kutafuta rasilimali zitakazowezesha vikundi vilivyopata vipate zaidi ili kukidhi mahitaji yao na vile ambavyo havijapata navyo vinufaike na huduma zetu,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment