Saturday, 13 September 2014

AFISA UVUVI WA WILAYA YA KILOLO AFARIKI KATIKA AJALI YA PIKIPIKI

RPC Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi
AFISA Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, William Mwazoka amepoteza maisha baada ya kugongwa na gari namba T789 BMF Mitsubishi Canter iliyokuwa ikiendeshwa na Ordo Leonard, mkazi wa Mtwivilla, mjini Iringa.

Wakati akipata ajali hiyo, Mwazoka alikuwa akiendesha pikipiki aina ya Honda yenye namba za usajili STL 483, mali ya halmashauri ya wilaya ya Kilolo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Pudenciana Protas alisema ajali hiyo ilitokea Septemba 10 majira saa 12.45 jioni katika barabara ya Kilolo- Iringa katika kijiji cha Kilolo.

Kamanda Protas alisema baada ya ajali hiyo, Afisa huyo alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa, mjini Iringa na kufariki Septemba 11, majira ya saa nane mchana wakati akiendelea na matibabu.

Katika tukio lingine, jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji lililotokea Septemba 11, majira ya saa 7:38 mchana katika kijiji cha Ng’ang’ange wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Kuhusu tukio hilo, Kaimu RPC alisema Kogura Kusige (19) mkazi wa kijiji hicho alipoteza maisha baada ya kupigwa kichwani na kitu chenye ncha butu.

Protas alisema; “Kusige alishambuliwa na watu wasiofahamika na kupigwa na kitu hicho kilichopasua fuvu la kichwa chake katika tukio tunaloendelea kulichunguza.”

Aliwataka wananchi wa kijiji hicho kusaidia na jeshi la Polisi kupata taarifa za watuhumiwa wa mauaji hayo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika tukio lingine, Kaimu RPC alisema jeshi la Polisi limemkamata na kumtia nguvuni Allein Aldo baada ya kukutwa na kete 19 za dawa za kulevyam aina ya Cocaine.

Alisema Aldo alikamatwa Septemba 11, majiraya saa 5.30 asubuhi wakati askari polisi wakiendelea na doria yao ya kawaida katika maeneo ya barabara mbili, mjini Iringa.

Alisema mtuhumiwa alikutwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya akiwa ameficha kwenye mfuko wa suruali aliyovaa katika harakati zake za kuwapelekea wateja wake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment