Friday, 29 August 2014

SERIKALI KUMALIZIA KIPORO CHA SENSA YA VIWANDA LUDEWA, NJOMBE

Fabian Fundi, Meneja Takwimu Iringa na Njombe
WIZARA ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu ya Taifa inamalizia kiporo kilichobaki wilayani Ludewa mkoani Njombe cha uorodheshaji wa viwanda kwa ajili ya sense ya viwanda inayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

“Kama mnavyokumbuka zoezi hili la uorodheshaji wa viwanda lilianza April 8, mwaka huu kwa Tanzania Bara ambapo maeneo yote kasoro wilaya ya Ludewa zoezi hili lilikamilika,” Meneja wa Takwimu Mkoa wa Iringa na Njombe, Fabian Fundi alisema.

Fundi alisema katika wilaya hiyo zoezi lilishindwa kukamilika kutokana na tarehe zilizokuwa zimepangwa kwa kazi hiyo kuingiliana na shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru.

Alisema ukamilishaji wa zoezi la uorodheshaji wa viwanda hivyo katika kata 16 za wilaya hiyo umeanza Agosti 25 na unatarajiwa kukamilika Agosti 31, mwaka huu.

 Fundi aliwataka wamiliki wa viwanda waliopo katika wilaya hiyo kutoa ushirikiano na taarifa sahihi kwa wadadisi watakaopita katika viwanda vyao kwa manufaa ya Taifa.

Alisema zoezi hilo litasaidia kupata picha halisi ya idadi ya viwanda katika ngazi ya kata na kijiji hasa kwa kuzingatia kwamba kwa mara ya mwisho sensa hiyo ilifanywa mwaka 1989 na kusaidia serikali kutambua sekta ya viwanda kujua  viko vingapi, idadi ya waajiri na waajiriwa wake, masoko yake, mchango wake kwa pato la taifa na mishahara wanayolipwa wafanyakazi wake.

Fundi alisema taarifa nyingine zitakazopatikana kupitia sensa hiyo  itakayohusisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ni pamoja na mwaka kiwanda kilipoanzishwa, aina ya bidhaa zinazozalishwa, gharama za uzalishaji,
jina la kiwanda, anuani ya kiwanda, mahali kiwanda kilipo, aina ya umiliki na utaifa wa mmiliki.


Alizitaja kata zitakazotembelewa na wadadisi kuwa ni kata ya Ludende, Lugarawa,Ruhuhu,Lupanga, Mundindi, Lwela,Mavanga,Ibumi, Mlangali, Kilondo,Madope,Lupingu, Madilu,Makonde, Mkongobaki na Lifuma

Reactions:

0 comments:

Post a Comment