Friday, 15 August 2014

KUTOKA MABANDA YA KINYWAJI NA VIJIWE VYA IRINGA MJINI; WASIOSIKIKA KARIBU NA MR HOTEL WATAKA TAA ZA BARABARANI IRINGA

Kazi ya ukarabati wa barabara ya Mista Hoteli Mkwawa ikiendelea
JANA Agosti 14 BONGO LEAKS ilitembelea kijiwe maarufu cha mgahawa wa Zanjabir.

Wanaokijua kijiwe hiki watakubaliana na BONGO LEAKS kwamba kina umaarufu mkubwa hasa kwa kuwa kina aina ya vitafunwa, supu na vyakula vinavyopikwa kwa ustadi mkubwa ikilinganishwa na vijiwe vya hadhi yake.

Ni kijiwe kinachokusanya mabibi na mabawana wakiwemo watu maarufu wa mjini Iringa hasa nyakati za jioni. Mishikaki, uji, supu ya pweza na vitafunwa aina kwa aina ni moja ya sababu inayoyapeleka makundi hayo ya watu hapo.

Kijiwe hiki kinatazama na ile hoteli maarufu ya MR wengi wamezoa kupaita Mista Hoteli; Mista hoteli ipo pembeni mwa barabara ya Mista hoteli-Mkwawa. Barabara hii ipo kwenye ukarabati, ni baada ya kufikia hatua ambayo viraka vyake vilikuwa havizibiki tena.

Katika kijiwe hicho BONGO LEAKS ikakutana na kundi la vijana wakinywa na kutafuna.

Wakati ikiendelea kula mishikaki mmoja wa vijana ASIYESIKIKA akasema…bora barabara hii inakarabatiwa na tumesikia kwamba ikikamilika zitawekwa taa za barabarani.

Akasema litakuwa jambo zuri maana mji huu unatia aibu, taa za barabara zipo lakini haziwashwi. Hata yalipo makao makuu ya manispaa ya Iringa ni aibu tupu, ukipita usiku utafikiri unapita pembeni ya msitu, pana kiza tororo kwasababu hapana taa za kutosha na barabarani yake iendayo yalipo makao makuu ya jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mahakama ya Mwanzo na Ofisi ya Shirika la Nyumba la Taifa hakuna taa hata moja ya barabarani, ASIYESIKIKA huyo alisema.

ASIYESIKIKA alisema bora waweka taa barabara hii ya Mista Hoteli maana ndiyo barabara inayotumiwa na wengi wakiwemo wale wa mabanda ya kitimoto yanayokusanya watu wengi hasa nyakati za usiku.

ASIYESIKIKA mwingine akauliza kwani inajengwa na nani? wa kwanza akajibu hata mimi sijui, mwingine akasema kama inajengwa na serikali ya CCM huenda ikawekwa taa za barabarani lakini kama inajengwa na Mbunge Mchungaji Peter Msigwa hiyo tusahau, tutaendelea kupita ikiwa na kiza kama tulivyozoea.

ASIYESIKIKA mwingine akadakia………aaha wewe Msigwa anawezaje kujenga barabara, mbona hiyo siyo kazi yake?, kazi yake ni kuisukuma serikali itekeleze ahadi zake na hiyo nadhani ndiyo kazi aliyofanya mpaka barabara hii ikaanza kukarabatiwa, kwahiyo kama mpango ni kuweka taa za barabarani ni lazima zitawekwa.

ASIYESIKIKA mwingine akadakia…… Msigwa hana issue, barabara hii itakuwa imejengwa na Ritta Kabati, maana angalau yeye tunamsikia bungeni akiongea juu ya maendeleo ya jimbo la Iringa Mjini. Huyu mwingine kazi yake ni moja tu Tembo na yeye, yeye na Tembo na hata bajeti ya kujenga barabara hii aliikataa akisema ni ndogo, au nyinyi hamjui hilo? aliuliza.

Itaendelea……………………………….


Reactions:

0 comments:

Post a Comment