Thursday, 14 August 2014

KUTOKA MABANDA YA KINYWAJI NA VIJIWE VYA IRINGA MJINI; WASIOSIKIKA MSHINDO WANENA KUHUSU UBUNGE 2015


JANA Agosti 13 BONGO LEAKS ilitembelea banda moja la kinywaji la mjini Iringa maarufu kama Sunga Grocery.

Grocery hii ipo jirani kabisa na kituo maarufu cha taxi cha mshindo jirani na benki ya NBC.

BONGO LEAKS akaungana na jamaa na kupata kinywaji; ilikuwa muda umepita baada ya wanahabari wa mkoa wa Iringa kuungana na familia ya Malangalila kuulaza katika nyumba yake ya milele, mwili wa mwanahabari Mkongwe Fulgance Malangalila.

Malangalila alikuwa mwandishi wa kujitegemea wa mjini Iringa, akifanya kazi na magazeti mbalimbali likiwemo gazeti la Business Times na Majira. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Malangalia ametuacha tukiwa tumejifunza mengi kutoka kwake, maarifa na uzoefu aliokuwa nao katika tasnia hii ulitosha kutufikisha baadhi yetu hapa tulipo.

Tulimuahidi akiwa hai na tunaendelea kumuahidi akiwa ametangulia mbele ya haki kwamba hatutaweka chini peni na kamera zetu katika kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi hii.

BONGO LEAKS ikiwa katika banda hilo, mengi yakazungumzwa kuhusu msiba huo kabla mada haijabadilika baada ya kijana mmoja kuingia akiwa amevaa kofia.

Haikuwa kofia kama zile zinazovaliwa na wale vijana wenzangu wanaovaa suruali zikiwa zinaning’inia chini ya kiuno. Ilikuwa kofia yenye rangi ya kijani na mbele yake ina picha.

WASIOSIKIKA wakabadili maongezi wakimkazia macho ASIYESIKA huyo ndani ya kofia yake. Eeeeh wewe umefuata nini…..toka bwana….kwani hakuna sehemu nyingine unaweza kunywa ukiwa na hiyo kofia yako? Mmoja kati ya WASIOSIKIKA hao alipaza sauti.

Kijana huyo hakuwa mnyonge, naye akawakazia macho na kutoa jibu lililoiacha BONGO LEAKS hoi kwa kicheko……eeeh kwendeni zenu huko kwanza pombe mnayokunywa mnaonkena mna mawazo, mnafikiri siasa ni kupalilia tu maisha ya wenzenu wakati nyinyi mnakunywa viroba hapa?

Kwani nyinyi hamtaki bia na kuku, hamtaki watoto wenu waende shule. Mbona mnawashabikia tu watu wasiotaka kukosolewa, wanaokula kwa mikono miwili na mnaoshindwa kuwatofautisha na wale mnaowatuhumu huku nyinyi mkichosha sura zenu kwa viroba.

Muulizeni mwenzenu yupo wapi? Kundi la WASIOSIKIKA likauliza nani? ASIYESIKA mwenye kofia akajibu Mchungaji Peter Msigwa, muulizeni kwanini anachukiwa ndani ya chama chake, muulizeni kwanini wenzake hawataki awe tena kiongozi wao, muulizeni kwanini anatumia hila kurudi katika uongozi wa chama, muulizeni kwanini haivi na mbunge mwenzake Chiku Abwao, muulizeni amewasadia vijana wangapi kuboresha shughuli zao, muulizeni wakili aliyeahidi kumlipa mshahara kwa ajili ya wanyonge yupo wapi, muulizeni kwanini anatukana wanahabari waliosaidia akafika hapo alipo, muulizeni ahadi zote alizotoa wakati wa uchaguzi mkuu katekeleza zipi, muulizeni kwanini ana roho mbaya husuda chuki jeuri kiburi asiyependa kukosolewa na aambiliki, muulizeni kwanini anashindwa hata kuboresha ofisi yao ya chama ya wilaya, muulizeni yeye ni mchungaji kwanini anatumia lugha zisizofaa dhidi ya wenzake, muulizeni atafanya na nani kampeni za 2015 kama ataendelea kuwa na mkono wa birika, muulizeni kama anajua mahitaji ya vijana, wanawake na wazee, muulizeni makundi hayo kayasaidia vipi, muulizeni jinsi alivyopata UBUNGE 2010 na kama itakuwa hivyo 2015.   

ASIYESIKIKA huyo akashika kofia yake na huku akiondoka akasema …nina waheshimu sana, acheni ushabiki, ushabiki wa kijinga, kama mnataka mabadiliko ni lazima yaanzie kwenu, tafuteni viongozi watakaojua mnataka nini na kusaidia mfike mnakotaka kwenda

WASIOSIKIKA waliobaki wakainamisha vichwa, BONGO LEAKS haikujua wanatafakari nini


Itaendelea……………………………….

Reactions:

0 comments:

Post a Comment