Saturday, 16 August 2014

HEPAUTWA CUP KUANZA KUTIMU VUMBI SAA 10 YA LEO KATIKA UWANJA WA SAMORA MJINI IRINGA


Nuru Hepautwa (mwenye miwani), mdhamini wa Hepautwa Cup alipokuwa akitoa vifaa kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo
Jezi za aina mbalimbali zilitolewa
Akiwa katika picha ya pamoja na timu zitakazoshiriki ligi hiyo
WAKATI wapenzi wa soka la Uingereza wakijiandaa hii leo kushuhudia ufunguzi wa ligi kuu ya taifa hilo, wale wapenzi wa soka wa mjini Iringa wanajiandaa kushuhudia ligi ya mtoano kuwania Kombe la Hepautwa.

Wakati Ligi Kuu ya Uingereza inatarajia kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini humo, ile ya Hepautwa itazinduliwa katika uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa saa 10 jioni leo.

Ligi Kombe la Hepautwa inatarajia kuvuta wapenzi wengi hasa baada ya mdhamini wake, Nuru Hepautwa kuboresha zawadi kwa washindi.

Mbali na Kombe la thamani, mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayokuwa ikichezwa kila mwaka kuanzia mwaka huu kwa lengo la kutafuta vipaji na kuongeza hamasa ya wakazi wa Iringa kuupenda mchezo huo ataondoka na Sh Milioni Moja taslimu.

Hepautwa alisema mshindi wa pili atalamba Sh 600,000 huku wa tatu akiondoka na Sh 300,000.

“Haijawahi kutokea ligi inayoshirikisha timu kutoka kwenye kata mshindi wake wa kwanza akaondoka na Sh Milioni moja,” alisema Athumani Hingison, mdau wa soka wa mjini Iringa.

Hingison alisema ligi nyingi ikiwemo ile inayoandaliwa na Frederick Mwakalebela na Mchungaji Peter Msigwa zawadi zake hazifikii za Ligi ya Hepautwa jambo linalofanya mashindano hayo yaonekane ya kipekee.

Wito wangu kwa wadau wa soka wa mjini Iringa ni kujitokeza kwa wingi kushuhudia ligi hiyo ambayo kiingilio chake ni bure, alisema Rashid Zongo ambaye ni mmoja wa viongozi wa soka wa manispaa ya Iringa.

Hepautwa alisema mafanikio yatakayojitokeza katika ligi hiyo mwaka huu yatamuongezea hamasa ya kuboresha zaidi zawadi kwa washindi na timu zote zinazoshiriki ambazo mwaka huu zimepata jezi kila moja.

Lengo letu ni kuhakikisha tunaibua vipaji ili kurudisha historia ya soka ya mkoa wa Iringa.
Alisema muda umefika kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kushikamana pamoja na kutumia rasilimali walizonazo kuhakikisha kwamba wanapata timu itakayoshiriki Ligi Kuu.

Kwa mara ya mwisho wakazi wa mkoa wa Iringa walishuhudia ligi kuu ikichezwa katika uwanja wake wa Samora mwaka 1999 kabla timu ya Lipuli iliyokuwa katika ligi hiyo haijashuka daraja na jitihada zake za kuirudisha kwenye ligi hiyo zikiendelea kugonga mwamba mwaka hadi mwaka.

Lipuli na pamoja na Kurugenzi Mufindi zinazoshiriki ligi daraja la kwanza ambayo ni hatua moja kabla ya kupanda ligi kuu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment