Wednesday, 2 July 2014

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAITETEA KAMPUNI ILIYOPEWA ZABUNI YA KUSAMBAZA VIFAA VYA KUANDIKISHA WAPIGA KURA

Jaji John Mkwawa

Baadhi ya wanahabari walioshiriki mkutano wa NEC
MCHAKATO wa kumpata mzabuni atakaye sambaza vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) kupitia mpango mpya wa tume hiyo wa kuboresha daftari la wapiga kura, umeelezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwamba ulifanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni za manunuzi.

Katika mkutano wa tume hiyo na wanahabari wa mjini Iringa uliofanyika katika ofisi ya mkuu wa mkoa jana, Kamishana wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu John Mkwawa alisema kampuni ya M/S Lithotech Exports ya Afrika Kusini ilishinda tenda hiyo kihalali.

Jaji Mkwawa alikuwa akikanusha taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii ambazo pia ziliwahi kuchapishwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kila siku siku za nyuma kwamba mchakato huo ulikuwa na harufu ya rushwa.

Alisema kampuni hiyo ilishinda tenda hiyo baada mchakato wa tume hiyo kurudiwa ikiwa ni matokeo ya kampuni aliyoitaja kwa jina la Morpho ya Ufaransa kukata rufaa ikipinga mchakato wa awali wa zabuni hiyo uliompa ushindi kampuni ya M/S SCI Tanzania Ltd.

Kampuni hiyo ilihoji njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya kuwa na uzoefu, vifaa bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama tofauti na kampuni iliyopewa kazi.

Kampuni zingine zinazodaiwa kuomba na kukosa kazi hiyo ni pamoja na M/S Zetes SA ya nchini Ubelgiji, M/S IRIS Corporation Technology ya Malaysia na M/S Avante International Technology, Inc ya Marerkani.

“Baada ya rufani hiyo tulilazimika kurudia mchakato wa kumpata mzabuni na niwahakikishieni kampuni hiyo iliyoshinda katika mchakato wa marudio ilipatikana kwa njia sahihi kwa kuzingatia sharia na kanuni zote za manunuzi,” alisema.

Alisema katika hatua za awali tume inaridhika na uwezo wa mzabuni huyo na ni imani yao kwamba hata wazabuni wengine wanamkubali na ndio maana hawakukuta rufaa.

Taarifa ya awali ya mchakato huo (iliyochapwa katika mitandao hiyo) inaonesha NEC iliingia katika mchakato wa mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.

Kampuni hizo ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zilitajwa kushirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited ambayo mwanzo ilishinda tenda hiyo, mbali ya kutojulikana zinapotoka, pia ndizo zilizokuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.

Kiwango ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3, wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.

Kwa mujibu wa Jaji Mkwawa NEc imekwishaanza mchakato wa uboreshaji wa dafatari hilo.

Alisema tume inatarajia kufanya uboreshaji wa daftari hilo kwa awamu ya kwanza hivi karibuni kwa kutumia tekenolijia hiyo ya Biometric Voter Registration.

"Ni matarajio yetu kwamba matumizi ya BVR yatapunguza au kuondoa kabisa matatizo yaliyomo kwenye daftari lililopo hivisasa ikiwepo kuzuia mtu mmoja kujiandikisha zaidi ya mara moja," alisema.

Alisema wapiga kura wote waliojiandikisha awali na wale wapya watalazimika kwenda vituoni kwa ajili ya kuandikishwa upya kwa maana ya kuchukuliwa taarifa za kibaiolojia, kubadili taarifa kwa wale waliohama au kubadili majina na kuandikisha wale wote ambao hawakujiandikisha hapo awali.

Alisema watu milioni 26 wanatarajiwa kuandikishwa nchini kote katika awamu hiyo ya kwanza ya uboreshaji wa daftari hilo na kwamba wapiga kura watakaotimiza miaka 18 ifikapo Oktoba 2015 nao watahusika katika uandikishaji huo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa mujibu wa Jaji Mkwawa inakisia kutumia zaidi ya Sh Bilioni 223 kukamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari hilo.

Aliwataka watanzania wote wenye sifa kutosubiri siku ya mwisho, pale shughuli ya uandikishaji itakapoanza. Siku 14 zimetengwa kwa ajili ya uandikishaji huo awamu ya kwanza.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment