Thursday, 3 July 2014

TANESCO YAOMBWA KUFUNGUA MAJI YALIYOZUIWA BWAWA LA MTERA

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerlad Guninita mwenye koti la rangi ya damu ya mzee pamoja na maafisa wengine wa wilaya hiyo walipokuwa katika bonde la mto Ruaha Mkuu; hivi ndivyo linavyoonekana kwasasa pamoja na mvua nyingi kunyesha msimu uliopita
Ukiwa katika kina chake huwezi kuvuka bila mitumbwi, lakini kwa hali ya sasa, unaweza kuvuka bonde hilo kwa kutembea kwa miguu au vyombo vya usafiri
WANANCHI wakulima wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda, wilayani Kilolo mkoani Iringa wameliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwanusuru kwa kuruhusu maji ya Mto Ruaha Mkuu kutililika katika mkondo wa mto huo.

Pamoja na msimu wa 2013/2014 kuwa na mvua nyingi katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa, ujazo wa maji katika bwawa la Mtera ambalo maji yake hutumika kuzalisha umeme wa grid ya Taifa haujafika katika kina chake.

Kwa mujibu wa Afisa wa Maji wa Bonde la Rufiji, Idrisa Msuya kina cha juu cha maji katika bwawa hilo kinachotakiwa kuzalisha umeme ni mita za ujazo 698.5; pamoja na mvua hizo kina chake mpaka sasqa kipo chini ya ujazo huo.

Hali hiyo imesababisha Tanesco kusimamisha uzalishaji wa umeme katika bwawa hilo na kufunga maji yanayotiririka kuelekea katika vijiji hivyo kwa kupitia bonde la mto Ruaha mkuu.

Uamuzi huo umeelezwa na baadhi ya wakulima wa vijiji hivyo kuhatarisha shughuli zao za kilimo cha umwagiliaji kinachotegemea maji yanayotiririka katika mto huo.

“Sehemu ya mto huo inayopita katika vijiji hivyo imekosa maji baada ya Shirika la Tanesco kuzuia maji yanayopita katika mto huo ili kuliwezesha Bwawa la Mtera kupata kiwango cha maji kinachostahili kuzalisha umeme,” alisema mmoja wa wakulima hao Boniface Mgwale.

Mgwale alisema pamoja na kuhatarisha kilimo hicho, wakulima hao wako katika hatari ya kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kutoka katika Benki ya Wananchi Mufindi (MUCOBA) ili iwasaidie kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wa zao la biashara la kitunguu.

Ili kuwanusuru wakulima na wananchi wengine wanaotegemea mto huo kwa shughuli za kilimo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita aliiomba Tanesco kuruhusu kwa muda maji yatiririke katika mto huo.


“Tunajua umuhimu wa bwawa la mtera katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini, lakini maji yanayopita katika mto huu, yanahitajika sana kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kwahiyo yote mawili ni muhimu yakafanyika,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment