Sunday, 13 July 2014

RAIS ATIMIZA AHADI YA KULETA WANAMUZIKI TOKA MAREKANI

Terrence J

Chaka Zulu
Ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa wasanii wa Tanzania kuwa atachangia kuinua kiwango cha ujuzi na weledi wao kwa kuwaandalia mafunzo yatayoendeshwa na magwiji wa sanaa kutoka Marekani sasa imetimia.

Akizindua Kampeni ya Uzalendo kwa Vijana inayoendeshwa na Muungano wa Wasanii Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma mwezi uliopita, Juni 14, 2014, Rais Kikwete aliahidi kuchangia kuinua kiwango cha usanii na weledi wa wasanii wa Tanzania kwa kusaidia kuandaa mafunzo yatakayoendeshwa na wasanii maarufu kutoka Marekani.

Katika kutimiza ahadi hiyo ya Rais Kikwete, kundi la wasanii kutoka Marekani limewasili nchini usiku wa Alhamisi, Julai 10, 2014, kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo yanayofanyika keshokutwa, Jumatatu, Julai 14, 2014, kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mjini Dar es Salaam. Kiasi cha wasanii 250 wamealikwa kushiriki semina hiyo inayoitwa Mafunzo ya Uendelezaji Usanii.

Wasanii ambao wako nchini kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo ni Chaka Zulu, Mtendaji wa Shughuli za Muziki kutoka Kampuni ya Disturbing The Peace Records na Davis Banner, mwigizaji, mwanamuziki, mtunzi na msimamizi wa shughuli za muziki ambaye amepata kushinda tuzo maarufu ya Grammy.

Wengine ni Terrence J. (Jenkins), mwendeshaji wa kipindi cha muziki kwenye televisheni ya E! Entertainment, mwigizaji wa filamu na mtunzi wa vitabu na Revi Shelton, Mtendaji wa Shughuli za Muziki katika Kampuni ya Outlet Media Group.

Mbali na kuendesha shughuli za mafunzo ya wasanii ambazo wamekuwa wakizifanya kwa makundi madogo madogo tokea walipowasili nchini, pia wanamuziki hao wa Marekani na kundi la wapiga picha watatembelea sehemu mbali mbali  nchini ambako watapiga picha na kuandaa vipindi vya kuitangaza Tanzania katika vyombo vya habari vya Marekani.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,

DAR ES SALAAM.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment