Saturday, 5 July 2014

MADENGE AIMWAGIA CCM JIMBO LA IRINGA MJINI MILIONI 24

Mahamudu Madenge
Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga
Baadhi ya mabalozi wa mtaa wa kihesa wakiwa katika semina hiyo
wakifuatilia mada

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC-CCM), Mahamudu Madenge ametoa Sh Milioni 24 zitakazotumika kuimarisha chama hicho jimbo la Iringa Mjini wakati kikijiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kiasi hicho cha fedha kwa mujibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga kitatumika kutoa semina kwa mabalozi wa nyumba kumi kumi wa kata zote 16 za jimbo hilo.

Semina hizo zitakazowafikia mabalozi zaidi ya 1,900 katika kata zote 16 za jimbo hilo zilianza jana katika kata za Kihesa na Nduli.

“Lengo la semina hizi ni kuwakumbusha mabalozi wetu wajibu wao kwa chama na wajibu wa chama kwao na kukijenga na kukiimarisha chama wakati tukielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema.

Mtenga ambaye pia ni Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa alisema chama hicho kina zaidi ya mabalozi 1,900.

Alisema mabalozi ni kitengo kinachotegemewa na chama hicho katika kuwaunganisha wanachama wake na ngazi mbalimbali za chama na viongozi wake.

“Semina hizi zimeanzia ngazi hii ya mabalozi, ni ngazi muhimu sana kwa maendeleo ya chama chetu…..baada ya hapo tutaendelea na semina hizo kwa wanachama na vingozi wa mashina, matawi, kata, umoja wa vijana na wanawake, jumuiya ya wazazi na viongozi ngazi ya wilaya,” alisema

Akimshukuru na kumpongeza Madenge kwa kukiwezesha chama kufanya semina hizo, Mtenga alisema ni kiongozi anayepaswa kuigwa kwasababu anajua na anatekeleza majukumu yake ya kichama kwa kuzingatia nafasi aliyonayo.

Alisema chama hicho kinaingia katika semina hizo kikiwa na mtaji wa wanachama zaidi ya 26,000 huku kikiendelea kupokea wengine ambao kwa pamoja wanatarajia kukiwezesha kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.  

Akizungumzia sababu ya kuchangia fedha hizo, Madenge alisema; “nilipochaguliwa kuwa MNEC kuiwakilisha manispaa hii niliahidi kutumia nguvu zangu zote kukijenga chama hiki.”

Alisema asipofanya hivyo atakuwa awasaliti wanachama wa chama hicho, waliomuamini na hatimaye kumpa jukumu zito katika chama hicho kwa kumchagua kuwa muwakilishi wao katika vikao vya NEC.

“Napokwenda kule na kwenye vikao vingine natakiwa niseme nimefanya kazi gani kwa kutumia nafasi yangu hii katika kukijenga chama, naamini wana CCM wa Manispaa ya Iringa hawakunichagua ili nitembee katika gari lenye bendera bila kufanya kazi yoyote ya chama,” alisema.

Alisema kwa kutumia nafasi aliyonayo katika chama hicho ataendelea kutafuta fedha ili semina kama hizo ziwafikie wanachama na viongozi wengine wote wa jimbo hilo ambalo kwa mwaka wa nne sasa linaongozwa na Mbunge kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment