Sunday, 6 July 2014

BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANI LATOA TAMKO LINGINE KUHUSU KATIBA MPYA, LASEMA HALIKO NYUMA YA KIONGOZI WALA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA

Rais wa Baraza Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa
Akisisitiza jambo
BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania limewatoa hofu watanzania katika tamko lake lingine kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) likisema haliko nyuma ya viongozi wala chama chochote cha siasa kama baadhi yao wanavyofiki.

Akitoa tamko hilo mjini Iringa jana, Rais wa Baraza hilo ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Iringa, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alisema; “Baraza la Maaskofu Katoliki halina chama katika hili, lakini pia halina mtu au mwanasiasa au chama linachokifanyia kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.”

Katika Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Ngalalekumtwa iliyofanyika mjini Iringa hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Baraza hilo, Askofu Severine Niwemugizi alitoa tamko kuhusu mchakato huo kwa kuwataka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi katika bunge hilo bila masharti.

April 16, mwaka huu, wajumbe wanaounda umoja huo, waliamua kutoka nje ya bunge hilo wakipinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa katika rasimu hiyo.

Katika tamko hilo Askofu Ngalalekumtwa alisema; “katika ujumbe wetu wa kichungaji wa Pasaka 2014, sisi maaskofu Katoliki Tanzania tuliwaandikia barua watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu tukiwaalika kuchukulia maanani mchakato wa kuandika katiba mpya.”

Alisema “wakati huu tunawaalika watanzania wote kwa pamoja, tuungane kuwakumbusha wale waliopewa dhamana ya kukamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba kuwajibika binafsi na katika maridhiano kutupatia katiba maridhawa.”

Alisema wajumbe wa bunge hilo wanapasa kujadili kwa umakini kila kilichopo katika rasimu hiyo ili wafikie muafaka utakaoenzi ujasiri wa kipekee wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wa kuanzisha mchakato huo.

“Tunawaasa tukiwaombea dhamiri zao zipate maoni mapya ili waweze kubeba kikamilifu dhamana hiyo waliyokabidhiwa,” alisema.

Askofu Ngalalekumtwa alisema baraza la maaskofu katoliki linawataka wajumbe  wa bunge hilo kuwa wamoja na kufanya kazi yao kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama.

Alisema ni mategemo yao majadiliano yatafanyika kwa kuheshimiana, kutumia hoja za kizalendo na kiungwana na kuyaangalia kwa mapana mambo na masuala makuu yaliyopendekezwa katika rasimu hiyo.

“Kuandika katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama, na hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda katiba mpya kwa kuzingatia Rasimu ya Pili utaweza kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu,” alisema.

Alisema kwa kadri nchi iliyivyo hivisasa kuna sababu za kutosha za kutaka Katiba mpya zikiwa ni pamoja na ufisadi, wananchi kujisikia kukosa usalama na amani, nchi kutokuwa na dira na tunu msingi.

“Na kwahiyo tunawasihi kwa mara nyingine tena ninyi wajumbe wa bunge hilo kurejea katika sehemu ya pili ya mjadala hapo mwezi Agosti mkiwa na moyo na mtazamo mpya,” alisema.

Alisema kwa kazi hiyo wajumbe hao watawasaidia watanzania waendelee kujivunia kuwa na taifa adilifu lenye amani na linalofanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya manufaa na ustawi wa wote.

Alisema ikiwa matokeo yatakuwa yenye kuleta mema na kuimarisha amani na utulivu wa nchi, watanzania wote watawashukuru na kuwasifu na kama tunda la kazi ya bunge hilo litakuwa ni lenye kuingiza nchi katika matatizo zaidi, kuwataabisha wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi watanzania watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika jukumu hilo muhimu mlilokabidhiwa.

Askofu Ngalalekumtwa alisema nchi haiko tayari kurudi nyuma na kuendelea na maisha yanayoongozwa na Katiba ya 1977 kwahiyo mahitaji ni kuwa na katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika maamuzi na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

“Tunataka Katiba ambayo inaruhusu utawala wa sheria, haki sawa kwa wote, manufaa na ustawi kwa wote na kuheshimu utu wa kila mmoja. Katiba shirikishi katika matumizi ya madaraka ili yatumike katika kuhudumia wote badala ya wachache na inayoweza kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi,” alisema.

Alipoulizwa msimamo wake nini kuhusu muundo wa serikali, Askofu Ngalalekumtwa alisema; “siwezi kusema popote pale, naogopa kuwapa ushawishi watu wetu na ndio maana msimamo wa kanisa ni kuwataka wajumbe wote warejee, wajadiliane na kutuletea katiba itakayokuwa na sifa hizo.”


Reactions:

0 comments:

Post a Comment