Thursday, 26 June 2014

TANESCO IRINGA YAOMBWA KUTENDA HAKI DHIDI YA WALALAMIKAJI HAWA

walalamikaji
WAKAZI wawili wa kijiji cha Tagamenda mjini Iringa, wameiomba Wizara ya Nishati na Madini kuwasaidia ili wapate fidia kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya kupitisha miradi ya umeme kwenye mashamba yao.

Shabani Mkakato na Kassim Mpingo kwa pamoja walizuiwa kuendelea na shughuli zozote katika mashamba yao yaliyopo jirani na kituo kidogo cha kuzalisha umeme cha Tagamenda, mjini Iringa baada ya Tanesco kupitisha miradi hiyo.

Wakizungumza na habarileo juzi walisema walipeleka maombi ya kufanyiwa tathimini na kulipwa fidia za mali na mimea iliyokuwa katika mashamba hayo lakini shirika hilo limewapa masharti yaliyo nje ya uwezo wao.

“Tulipeka barua kwa meneja wa Tanesco mkoa wa Iringa na katika majibu yake tunahisi haki yetu itapotea,” alisema Mkakato.

Akifafanua kuhusu miradi hiyo, Mpingo alisema ni ya umeme unaokwenda Ifunda, Sabasaba, Isimani na Cotex.

Alisema wakati nguzo nne zilipitishwa katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja, nyingine nne zilipitishwa kwenye shamba la mlalamikaji mwenzake Mkakato.

Alisema maeneo hayo ambayo hajapimwa walikuwa wanayamiliki kimila lakini walilazimika kuondoka baada ya kutolewa maagizo hayo ikiwa ni kupisha ujenzi wa miradi hiyo.

“Katika mashamba hayo kulikuwa na miti ya kupandwa, ya matunda na mazao mengine mbalimbali kama mahindi, mikunde na maharage,” Mpingo alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Tagamenda, Mwagike Mwagike alithibitisha watu hao kumiliki maeneo hayo kabla miradi hiyo ya Tanesco haijapitishwa.

“Nachofahamu ni kwamba watu wengine waliopitiwa na miradi hiyo katika eneo hilo walikwishalipwa fidia zao, sasa sijui wakati wa tathimini na malipo hayo hawa walikuwa wapi?” alisema.

Katika majibu yake kwa watu hao aliyoyatoa kupitia barua ya Mei 22, mwaka huu ikiwa na kumbukumbu Na RM/IRA/CUST/2 Meneja wa Tanesco Mkoa wa Iringa, Mhandisi Sarah Assey anasema wameshindwa kuyashughulikia madai hayo kwasababu ya maombo ya walalamikaji hao kutojitosheleza.

“Hujatueleza ni lini nguzo hizo zimewekwa kwenye eneo husika na zinahusika na mradi upi wa umeme. Kwa barua hii basi tunaomba utufahamishe ni mwaka gani nguzo hizo zimewekwa kwenye eneo hilo na zinaelekea wapi ili kama shirika tuweze kuyafanyia kazi madai yako,” inasomeka barua ya Tanesco iliyoandikwa kwa Mpingo.


Mpingo alisema mgogoro uliopo na ambao wanaohofia unaweza kukwamisha upatikanaji wa haki zao ni kipengele kilichopo katika barua ya meneja huyo kinachotaka walalamikaji hao waambatanishe kivuli cha hati miliki ya eneo husika, wakati maeneo hayo wao walikuwa wakiyamiliki maeneo hao kimila kwa kuwa hayajapimwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment