Friday, 27 June 2014

SPANEST KUFADHILI LIGI SOKA KWA VIJANA WA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA, ITAANZA JUNI 28, LENGO KUWAELIMISHA KUPINGA UJANGILI

Mratibu wa Spanest, Godwell Olle Meing'araki akionesha kikombe kitakachogombaniwa katika ligi ya SPANEST 2014; ligi hiyo inalenga kuhamasisha vijana  wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha kupinga ujangili

Akionesha medali kwa mshindi wa kwanza
Akionesha moja ya mipira itakayotumika katika ligi hiyo na kutolewa kama zawadi kwa washindi
Akisisitiza jambo, huku katibu wa Chama cha Mapira wa Miguu Wilaya ya Iringa (IDFA), Juma Lalika akisikiliza
VIJANA wa vijiji 21 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wameingizwa katika kampeni za uhifadhi  na vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori kupitia mashindano  ya mpira wa miguu yanayoanza kufanyika Juni 28, mwaka huu.

Mashindano hayo yatakayosimamiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Iringa (IDFA), yatafanyika kwa uratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Hifadhi zilizoko Kusini mwa Tanzania (Spanest).

Katibu wa  IDFA, Juma Lalika alisema mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kila mwaka kuanzia mwaka huu, yatajulikana kwa jina la “Ligi ya Kombe la Spanest” na yatashirikisha vijiji hivyo vinavyounda tarafa ya Idodi na Pawaga wilayani Iringa.

Mratibu wa Spanest, Godwell Olle Meing’ataki aliyataja malengo mahususi ya ligi hiyo kuwa ni kujenga uelewa juu ya uhifadhi wa wanyamapori miongoni mwa jamii ya vijiji jirani na hifadhi na kujenga mtizamo chanya kuhusu uhifadhi wa wanyamapori.

Menine ni kuinua vipaji kwa vijana wanaoishi jirani na hifadhi na kutoa burudani kwa jamii inayoishi jirani na hifadhi.

Alisema wadau mbalimbali wa uhifadhi wamechangia fedha zinazotokana na utalii wa wanyamapori kwa ajili ya kombe hilo linalotarajiwa kuwapa vijana hamasa ya kutafuta fursa zingine za maendeleo badala ya kufanya ujangili.

Alisema ujumbe muhimu wa ligi hiyo utakuwa "Piga Vita Ujangili, Piga Mpira, Okoa Tembo." 

Alizitaja zawadi zitakazotolewa kuwa ni pamoja na kikombe, medali ya dhahabu, seti moja ya jezi na fedha taslimu Sh 300,000 kwa mshindi wa kwanza.

Zawadi nyingine zitakazotolewa kwa mshindi huyo ni cheti na safari ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na kucheza mechi ya kirafiki.

Alisema mshindi wa pili atapata medali ya shaba, mipira miwili, cheti na Sh 200,000 taslimu huku mshindi wa tatu akipata medali ya shaba, cheti na Sh 100,000 na mshindi wa nne atapata kifuta jasho cha Sh 50,000.

Alisema watu wakitambua umuhimu wa wanyamapori na kusaidia kuwahifadhi watachochea ongezeko la watalii na upatikanaji wa fedha zikiwemo za kigeni zitakazosaidia pia kuboresha miradi mbalimbali ya jamii inayozunguka hifadhi hiyo kama ujenzi wa madarasa, mabweni, zahanati, miradi ya maji, ufugaji wa nyuki na uhifadhi za mazingira.

Alisema wanyamapori na mazingira waliyopo vikihifadhiwa wawekezaji wataendelea kujitokeza na kujenga hoteli za kitalii zitakazotoa ajira za moja kwa moja kwa wenyeji na kuwahamasisha wengine  kuingia katika biashara ya uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwa wageni vikiwemo vyakula vya kienyeji na vitu vya kitamaduni na hatimaye kustawisha jamii.

Meing’ataki alisema katika kupinga ujangili wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili imeonekana ni moja ya njia muafaka  kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.


“Takwimu za ujangili katika maeneo yaliyohifadhiwa zinaonesha kuwa vijana wengi hukamatwa katika matukio ya ujangili. Watu wenye fedha kutoka maeneo mbalimbali nchini huwarubuni vijana kwa fedha ili wakafanye ujangili kama vile wa tembo na wengine,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment