Thursday, 12 June 2014

REDDS MISS IRINGA KUFANYIKA JUNI 20, WAREMBO WAJIFUA ILE MBAYA

Baadhi ya warembo watakaoshiriki Redds Miss Iringa 2014 wakiwa katika pozi na Redds Miss Iringa 2013, Neema Mality

walimu wa walimbwende hao katika pozi wakati wa mazoezi yao
Mratibu wa Redds Miss Iringa 2014, Victor Chakudika akisisitiza mambo yatakuwa powa
WAKAZI wa mkoa wa Iringa, vijiji, mitaa na vitongoji vyake wanasubiri kwa hamu kushuhudia shindano la ulimbwende litakalomtoa Miss Iringa 2014.

Awali shindano hilo lilikuwa lifanyike Juni 6, mwaka huu, lakini likaahirishwa hadi Juni 20 baada ya aliyekuwa mratibu wake, Mohamed Mcholeka kuingia mitini.

Katika kunusuru shindano hilo na kukata kiu ya wapenzi wa mashindano ya ulimbwende, waandaji wakuu wa Redds Miss Tanzania chini ya Kampuni ya Lino Agency wameipa dhamana kampuni ya Chakudika Entertainment kuratibu shindano hilo.

Kampuni hiyo inamilikiwa na meneja wa redio maarufu ya mjini Iringa ya Nuru FM, Victor Chakudika.

Ili kufanikisha shindano hilo, Chakudika amewataka wakazi wa mkoa wa Iringa kujitokeza kwa wingi ili kulinda heshima ya shindano hilo.

Shindano la Redds Miss Iringa limekuwa likisaidia kuibua vipaji vya washiriki wanaojitokeza kila mwaka, kuongeza mzunguko wa pesa na ajira.

“Wapo warembo wanaopata ajira kupitia mashindano haya, lakini pia huwaongezea fursa za kielimu na kibiashara na kuwaongezea chachu ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusu jamii inayowazunguka,” amesema.

Chakudika amesema kampuni yake inaendelea na maandalizi ya kukata kwa shoka ili kuwafanya wadau watakaojitokeza kushuhudia waondoke wakiwa na nyoyo zilizoridhika.

Amesema shindano hilo litakalokuwa na burudani kedekede kutoka kwa msanii Mo Music anayetamba na wimbo wake wa Basi Nenda pamoja na wasanii wengine wa ndani na nje ya mkoa wa Iringa litafanyika katika ukumbi wa St Dominic mjini Iringa.

Amesema warembo 12 waliojitokeza kushiriki shindano hilo wanaendelea na mazoezi ya kufa mtu katika ukumbi wa Hoteli ya Gentle Hill ya mjini Iringa.


Redds Miss Iringa 2014 inadhaminiwa na kampuni ya Bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha Redds.


Wadhamini wengine ni pamoja na Nuru Fm, kampuni mpya ya mabasi ya Sutco High Class, Gentle Hills na J Marcs Barber shop.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment