Monday, 2 June 2014

MWIGULU AUMEZEA MATE URAIS ILI AWAFUNZE WAKOROFI ADABU, ATANGAZA KIAMA JIMBO LA IRINGA MJINI

MWIGULU NCHEMBA NA DK PINDI CHANA WAKICHANA MISTARI
BILA kutangaza nia, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha ameonesha kuumezea mate urais.

Nchemba alijipammbanua kuitamani nafasi hiyo jana alipokuwa akihutubia wafuasi lukuki wa chama hicho waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa, mjini Iringa.

Pamoja na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM, viongozi mbalimbali wa CCM waliopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo walielezea mkakati wa kummaliza kisiasa mbunge wa jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).

Akizungumzia sura ya uchaguzi mkuu wa 2015, Mwigulu alisema: “Natamani siku moja niongoze taifa hili ili niwafundishe watu kuwa na adabu.”

Alisema katika mazingira ya kawaida inawezekana watoto wakatukanana lakini litakuwa jambo la ukosefu wa adabu kama mtoto atamtukana baba yake na watu wazima wakashangilia vitendo hivyo.

“Hawa watu wanaojiita Ukawa hawana adabu, wanapaswa kufundishwa adabu, ni jambo la kushanga wanapoachwa tu wawatukane waasisi wa Taifa hili,” alisema.

Alisema katika bunge la jamhuri, baraza la wawakilishi na lile maalumu la Katiba hakuna mtu mwenye hadhi inayofanya na ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

“Tuwe wakweli tu, hakuna hata mmoja anayeweza kujifananisha na Mwalimu Nyerere, kwahiyo kumtukana sio tu anayefanya hivyo anajivunjia heshima yeye mwenyewe lakini pia analifedhehesha Taifa,” alisema.

Akizungumzia jimbo la Iringa Mjini alisema siku za mbunge huyo kuendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa nafasi hiyo zinahesabika.

“Tunawahakikishia tutashinda kwa kishindo; tutamshughulikia  Msigwa na hataamini yatakayomkuta kwasababu kilichompa ushindi mwaka 2010 ndicho kitakachomnyima ushindi huo katika uchaguzi mkuu ujao,” alisema.

Nchemba aliwasihi vijana wanaobandikwa jina la Makamanda kutafakari kwa kina sababu za kuitwa hivyo na hatma ya maisha na maendeleo yao kupitia kauli za viongozi wa Chadema.

“Huyu mtu anashindwa hata kuchangia vikundi vya akina mama lishe, bodaboda na vingine vingi vinavyohitaji misaada ya wadau ili vipige hatua zaidi,” alisema.

Kwa kuogopa kuulizwa maswali ya mchango wake wa maendeleo kwa shughuli za wananchi amekuwa akihamasisha vijana kuandamana na kufanya vurugu ili wasipate muda wa kukaa pamoja na kuulizana alichofanya tangu achaguliwe.

“Mpaka lini mtaendelea kuitwa makamanda kwa kupewa viroba; wenzenu wanatafuta maendeleo na muhimu viongozi mnaowachagua wakawaunga mkono,” alisema.

Akitoa mfano wa mbunge mwenye muda mfupi kabisa bungeni, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa alisema katika kipindi kifupi tangu aapishwe kushika nafasi hiyo ameanza kuonesha fadhila kwa wapiga kura wake kwa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Amechangia mabati, sementi, tofali na vitu vingi kwa watu wake wa Kalenga katika kipindi kifupi cha ubunge wake; huyu wenu kazi yake kulalamika na kukimbia shughuli za maendeleo mnazozifanya,” alisema.

Kauli ya Nchemba ilichagizwa na Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga aliyesema; “Msigwa atake asitake, ni lazima mwaka 2015 atang’oka.”

Mtenga alisema CCM imemleta mkoani Iringa huku ikijua kwamba mkoa huo ni wa chama hicho; ili kuondoa dosari ya kuwa na mbunge kupitia upinzani siasa itapigwa kuhakikisha anang’oka.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema CCM haitakubali kutoa lifti nyingine kwa mbunge huyo kwaababu madhara yake yanajulikana kwa wakazi wa jimbo la Iringa mjini.

“Hana analofanya bungeni zaidi ya kulalamika, akitoka nje anawafundisha vijana kuwachukia wazazi wao na kutuhatarishia amani ya nchi,” alisema.

Mbali na viongozi hao mkutano huo ulihudhuriwa na wabunge na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa na Naibu wa Waziri wa Wanawake, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.

Katika mkutano huo, Pindi Chana alimfananisha Mchungaji Msigwa na watoto wadogo wanaosusa kula pale wazazi wao wanaposhindwa kuwanunulia vitu wanavyotaka.

“Jiulizeni watu mnaowatuma kuwawakilisheni kwanini wakishindwa hoja wanatoka nje ya vikao, wanataka kutumia njia gani kuwasilisheni kero zenu; kiujumla hawatufai,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment