Thursday, 5 June 2014

MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO MUFINDI WAPEWA PIKIPIKI

Jaji Mary Shanghai akikata utepe wakati akikabidhi pikipiki hizo

Pikipiki zilizotolewa kwa mahakimu wa mahakama hizo
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shanghai amekabidhi pikipiki nne kwa mahakimu wa mahakama za mwanzo za Ifwagi na Kibao, Malangali, Kasanga na Mgololo, zote za wilaya ya Mufindi.

Kutolewa kwa pikipiki hizo, kumeelezwa na mahakimu wa mahakama hizo kwamba kutarahisisha utendaji kazi wao na kuongeza ufanisi katika idara hiyo muhimu ya utoaji haki.

Jaji Shanghai alikabidhi pikipiki hizo juzi katika ziara yake ya a kufahamiana na watendaji wa mahakama na kukagua shughuli mbalimbali za mahakama zinazofanywa wilayani humo.

Katika ziara hiyo, Shanghai alitembelea mahakamaa ya wilaya ya Mufindi na mahakama ya mwanzo Mafinga, Sadani, Mlangali, na Iramba.

Akisoma taarifa ya jumla ya mahakama ya wilaya hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi  Mfawidhi, Victoria Nongwa alisema mahakama hiyo inasimamia jumla ya mahakama za mwanzo zilizoko katika maeneo mbalimbali wilayani Mufindi.

Alizitaja mahakama hizo kuwa ni Mahakama ya Mafinga mjini, Mufindi (Kibaoni), Kasanga (Igowole) Malangali (Isimikinyi), Kibengu, Mapanda, Sadani (Utosi), Iramba (Itulavanu) Mgololo, Ihanu (Ibwanzi) na Ifwagi.

Alisema mahakama hiyo isiyo na mhasibu ina watumishi wa kada mbalimbali 31 ambao kati yao wanne ni mahakimu wakazi wa mahakama ya wilaya na watatu ni mahakimu wakazi wa mahakama za mwanzo.

Aliwataja watumishi wengine kuwa ni mahakimu watatu wa mahakama za mwanzo wasio mahakimu wakazi, mahafisa kumbukumbu watano ,wapiga chapa wawili, wahudumu wanne, walinzi nane na dereva mmoja.

Katika kuboresha utendaji wa mahakama hiyo, Nongwa ameomba msaada wa ujenzi wa mahakama ya mwanzo Ifwagi na ukarabati wa nyumba ya hakimu wake.

Wakati mjini Mafinga panatakiwa kujengwa upya mahakama yake ya mwanzo, alizitaja mahakama zingine zinazohitaji ukarabati kuwa ni Mufindi (Kibao), Kasanga (Igowole) na Malangali inayotakiwa kukarabatiwa choo na jengo la kutunzia vielezo.

Alisema mahakama hiyo inahitaji pia kujengewa chumba cha mahabusu Malangali na fedha ya kuwezesha kupatikana kwa umeme mbadala katika mahakama ya mwanzo Kibengu

Pamoja na maombi hayo, wazee wa baraza la Mahakama ya Mwanzo Mafinga wameulalamikia uongozi wa mahakama ya Wilaya hiyo kwa kutowalipa fedha zao za vikao vinavyohusisha kesi zilizofutwa.

Akiwatia moyo kwa kazi wanazofanya Jaji Shanghai alisema: “kuanzia sasa baraza la wazee litalipwa fedha zao kwa wakati hata kama kesi wanazohudhuria zitahirishwa au kufutwa.

Akizungumzia utendaji wa mahakama, Shaghai aliwaomba  mahakimu  kujiepusha na rushwa kwa kuwa ni moja ya sababu inayokwamisha upatikanaji wa haki katika chombo hicho.

Aliahidi kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kukabiliana na watendaji wenye tabia za kuomba na kupokea rushwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment