Wednesday, 11 June 2014

HIFADHI YA RUAHA YAIPIGIA MAGOTI SERIKALI, YAOMBA UMEME WA GRIDI

Dk Chris Timbuka
HIFADHI ya Taifa ya Ruaha imeiangukia serikali ikiomba ifikishiwe umeme wa gridi ya Taifa ili kupunguza gharama zake za uendeshaji.

Pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk Chris Timbuka alisema huduma hiyo itaharakisha mipango yao ya uboreshaji wa huduma za kitalii na uhifadhi, hifadhini humo.

Akizungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo hivikaribuni wakiwa na baadhi ya maafisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Timbuka alisema; ‘hifadhi ina mahitaji makubwa ya nishati hiyo na katika kupunguza makali yake tunatumia jenereta.”

Alisema wanatumia zaidi ya Sh Milioni 400 kila mwaka kununua mafuta ya jenereta zinazotumika kuzalisha umeme hifadhi hapo.

“Huu ni mzigo mkubwa, ni mkubwa kwasababu hifadhi hii bado haijafikia hatua ya kujiendesha kutokana na makusanyo ya mapato yake,” alisema.

Alisema sehemu kubwa ya bajeti ya matumizi ya hifadhi hiyo inategemea mapato yanayokusanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutoka baadhi ya hifadhi za mikoa ya kaskazini zinazojiendesha kwa faida.

“Tunaomba serikali ifikishe umeme hadi geti kuu la kuingilia hifadhini; tutakachofanya baada ya hapo ni kupitisha umeme huo ardhini hadi katika maeneo yote yenye mahitaji ya nishati hiyo,” alisema.

Taarifa zisizo rasmi ambazo hata hivyo zimekanushwa na mhifadhi huyo zinadai kwamba kulikuwepo na mpango  katika mwaka huu wa fedha wa kufikisha umeme wa gridi katika hifadhi hiyo hata hivyo uamuzi huo ulitenguliwa.

Mmoja wa watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) aliyekataa kutaja jina lake gazetini alisema; “kwa kupitia Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini yaani REA kulikuwa na mpango mwaka huu wa fedha wa kufikisha umeme katika hifadhi hiyo, hata hivyo mpango huo ulibadilishwa baadaye.”

Mmoja wa viongozi wa shirika hilo mkoani Iringa ambaye pia hakutaka kutaja jina lake gazetini kwa madai kwamba si msemaji alikanusha madai hayo.

Kiongozi huyo alisema wao kama wasimamizi wa miradi ya umeme inayotekelezwa kupitia mpango wa REA hawana taarifa mpango wowote wa nishati hiyo kupelekwa katika hifadhi hiyo mwaka huu wa fedha.

“Tunachofahamu ni kwamba nishai hiyo inaendelea kusambazwa katika cijiji vinavyopitiwa na barabara inayokwenda katika hifadhi hiyo kwa kutokea Iringa mjini; mpango unaonesha nishati hiyo haitafika hifadhini pamoja na kuepelekwa hadi vijiji vya Tungamalenga na Mauninga vilivyopo jirani kabisa na hifadhi hiyo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment