Tuesday, 10 June 2014

CHAMA KIPYA CHA WAFANYAKAZI WA VYOMBO VYA HABARI CHAJA

Wanahabari wa Tanzania katika moja ya maandamano yao ya kudai haki zao kama wafanyakazi huru nchini
KWA msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), wanahabari wa Tanzania wamerudi kwenye jitihada zao za kupata chama chao cha wafanyakazi.

Azimio hilo lilifanywa hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya baadhi ya wanahabari wa Tanzania kushiriki warsha ya siku mbili iliyohusu maendeleo ya vyama vya wafanyakazi.  

Washiriki katika warsha hiyo walichagua wajumbe watano watakaotengeneza katiba na kufuatilia maazimio ya mkutano huo ikiwa ni pamoja na kufanya usajili wa chama kipya kitakachojulikana kama “Journalists Union of Tanzania-JUT” au “Umoja wa Wanahabari wa Tanzania”.

Kwa muda mrefu, wanahabari wa Tanzania wameendelea kufanya kazi bila kuwa na chama chao cha wafanyakazi baada ya chama chao kilichokuwa na jukumu hilo cha Tanzania Union of Journalists (TUJ) kulegalega kutokana uongozi legelege.

TUJ ilifutwa katika orodha ya vyama vya wafanyakazi nchini Juni 24, 2013 baada ya kushitakiwa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mrajisi wa Vyama vya Wafanyakazi.


Waliochaguliwa kuunda kamati ya Katiba ni Samson Kamalamo, Timothy Kitundu, Jane Mihanji ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Umoja wa Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC) Arodia Peter na Hamisi Mzee kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment