Friday, 20 June 2014

CCM YAIHOFIA CHADEMA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA MIGORI KWA LUKUVI


Edward Mpangala, mwenyekiti wa kijiji cha Mbweleli
Shina la wakereketwa wa CCM na wafurukutwa wa Chadema
BAADHI ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kata ya Migori, jimbo la Isimani wilayani Iringa mkoani Iringa wanaohufu ya kupoteza serikali za vijiji vyao kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.

Kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote, uchaguzi huo utafanyika nchini kote Novemba mwaka huu.

“Hali ni mbaya, Chadema wanatupiga bao, vijana wengi wanakimbilia katika chama chao, tunatakiwa kujipanga ili tusipoteze kitu katika uchaguzi huo,” alisema Mwenyekiti wa kijiji cha Mbweleli, Edward Mpangala.

Mpangala alisema kwa bahati mbaya Chadema wanatumia siasa za ulaghai, uzushi na uongo uliopitiliza kuwashawishi vijana kujiunga na chama chao.

Na wakati hayo yakifanyika alisema wana CCM kwa upande wao wanaishi kama wanasinzia kwani wanashindwa kujibu mapigo.

Katika tukio la hivikaribuni, Mpangala alisema vijana wa chama hicho kijijini hapo waliituhumu uongozi wa serikali yake ya kijiji kuuza tofali za kijiji na kutafuna fedha zilizopatikana.

“Zilikuwa taarifa za uzushi, uongo na zilizojaa fitina, kwa bahati mbaya badala ya wana CCM kukaa pamoja na kushirikiana kuzikanusha baadhi yao wanazifurahia,” alisema.

Alisema uzushi huo unakiweka chama chao katika hatari ya kuangushwa na Chadema katika uchaguzi huo na akawataka wana CCM washikamane ili kuinusuru hali hiyo.

Akizungumzia ukweli kuhusu tukio hilo, Mpangala alisema: “tuliuza tanuru moja la tofali ili kulipa sehemu ya deni la Sh 550,000 tunalodaiwa na mwanakijiji mwenzetu Mika Koturo.

Alisema Kotoro alikikopesha kijiji hicho kiasi hicho cha fedha ili kiweze kufungua kaunti ya kijiji.

Alisema ili kulipa deni hilo la muda mrefu walilazimika kuuza tofali hizo zilizokuwa zitumike kwa ujenzi wa nyumba za walimu wa shule za msingi Mbweleli.

“Hata hivyo tofali hizo tuliuza kwa Sh 250,000 na zote zililipwa kwa muhusika ambaye bado anatutadi Sh 300,000,” alisema.

Alisema walilazimika kuuza tofali hizo kwasababu kijiji chao hakina vyanzo vya uhakika vya mapato.

Aliwatuhumu wana Chadema kwa kuwahamasisha wananchi kukataa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo kijijini hapo kupitia michango ya hiari na ile ya lazima ikiwemo inayotokana na tozo (ushuru) mbalimbali.

“Wananchi hawataki kulipa ushuru wa mazao, hawalipi ushuru wa biashara ndogondogo, hawalipi ushuru  wa pombe, samaki na wanakataa kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema.

Alisema mapato pekee ambayo  kijiji hicho inategemea ni yale yatokanayo na ushuru wa misitu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment