Wednesday, 25 June 2014

ASASI YA MUFINDI VIJANA KWA MAENDELEO YAIPIGA JEKI HOSPITALI YA WILAYA YA MUFINDI, MGANGA MKUU AELEZA KERO ZAKE NYINGI

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Goodluck Mlimbila alikijaribu kusukuma moja kati ya viti 33 vilivyotolewa na asasi ya MUVIMA kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Mufindi. Anayefurahi katikati ni mkurugenzi mwenza wa MUVIMA, Albert Chalamila akipongezwa na Katibu wa Afya wa Wilaya hiyo, Atupekisye Mwakifamba

Albert Chalamila na baadhi ya wanahabari wakiangalia hali ilivyo ndani ya wodi ya wazazi ya hospitali hiyo; hapa wanaonekana baadhi ya wajawazito wanaolala chini kutokana na ukosefu wa vitanda
Hapa akionesha maboksi yenye viti hivyo
Hapa Mkurugenzi wa MUVIMA, Chalamila akitembezwa katika mazingira ya hospitali hiyo
Hapa ni nje ya wodi ya wazazi
Na hiki ni moja kati ya viti vilivyokuwa vinatumiwa na hospitali hiyo kubeba wagonjwa
ASASI ya Mufindi Vijana kwa Maendeleo (MUVIMA) imeikabidhi hospitali ya wilaya ya Mufindi yenye matatizo mbalimbali  yanayofifisha utoaji wa huduma bora za afya, zikiwemo zile za wajawazito na watoto, msaada wa viti 33 vya kubeba wagonjwa.

Viti hivyo vya magurudumu matatu, vimeelezwa na Kaimu Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Dk Goodluck Mlimbila kwamba vitapunguza adha waliyokuwa wanapata watoa huduma wa hospitali hiyo ya kupokea na kubeba mikononi, wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Akikabidhi msaada huo juzi, Mkurugenzi Mwenza wa MUVIMA, Albert Chalamila alisema asasi yao imeguswa na kero mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo na kwa kuanzia ililazimika kutafuta viti hivyo.

“Tulikaa chini na kutengeneza andiko lililokubaliwa na asasi ya kimataifa ya Rafiki Surgical Mission ya Australia iliyotoa viti hivi; katika andiko letu hilo tumeomba pia tuisaidiwe vitanda kwa ajili ya hospitali hii; vitanda hivo 23 vimekwishawasili bandari ya Dar es Salaam” alisema.

Alisema Mkurugenzi Mkuu wa MUVIMA, Cosato Chumi anaendelea na utaratibu wa kuvitoa vitanda hivyo bandarini na mara baada ya shughuli hiyo kukamilika vitakavifdhiwa kwa uongozi wa hospitali hiyo.

Akishukuru kwa msaada huo, Dk Mlimbila alisema hospitali hiyo ina upungufu mkubwa wa vifaatiba na dawa na akalitaja eneo lenye tatizo zaidi kuwa ni lile la huduma kwa mjamzito na watoto.

Alisema katika kuboresha huduma za uzazi, jengo lenye uwezo wa kulaza wajawazito zaidi ya 100 na lenye chumba cha upasuaji na kile cha kuhifadhia watoto wanaozaliwa kabla ya muda lilijengwa katika hospitali hiyo ambayo awali ilikuwa ikitumia jengo lenye uwezo wa kuweka vitanda 27 tu.

“Huduma katika jengo hilo jipya zimeanza Mei mwaka huu, mpaka sasa lina vitanda 27 tu vya kulaza wajawazito wanaosubiri kujifungua na waliojifungua vilivyotolewa jengo la zamani; pamoja na kukosa vifaa vya  huduma ya upasuaji halina pia vifaa vya kuhifadhia watoto wanaojifungua kabla ya muda wao,” alisema.

Wakiwa katika mazingira hayo, wajawazito wengi wanalazimika kulala chini huku wanaobahatika kupata vitanda hivyo wakilala wawili kwa kila kitanda.

Alisema hali mbaya ya utoaji huduma kwa wajawazito inasababisha asilimia 29 ya vizazi hai 100,000 vya watoto, kufa kabla, wakati au baada ya kujifungua.

Alisema msaada uliotolewa na MUVIMA una umuhimu mkubwa katika hospitali hiyo kwani utarahisisha huduma za ubebaji wagonjwa kutoka eneo moja hadi lingine na utapunguza idadi ya wajawazito wanaolala chini baada ya vitanda vilivyoahidiwa kuwasili.

Naye Katibu wa Afya wa wilaya hiyo, Atupakisye Mwakifamba aliwataka MUVIMA na wadau wengi kujitokeza kuzimaliza kero za utoaji huduma zinazoikabili hospitali hiyo na vituo vingine vingi vya huduma wilayani humo.

Mwakifamba alisema pamoja na wilaya hiyo kuwa na idadi ya kuridhisha ya wato huduma wenye ujuzi, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa tiba, dawa na magari ya kubeba wagonjwa.


Wilaya ya Mufindi ni moja kati ya wilaya tatu zinazounda mkoa wa Iringa ikiwa na hospitali moja, vituo vya afya sita na zahanati 53. Pamoja idadi hiyo ya vutuo vya huduma ina magari matatu tu ya kubeba wagonjwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment