Monday, 23 June 2014

AFISA MISITU WILAYA YA KILOLO AKUMBWA NA TUHUMA NZITO, NI ZILE ZINAZOMUHUSIHA NA WIZI WA MITI YA MBAO KATIKA MSITU WA HALMASHAURI


Godfrey Mwita, Afisa Misitu wa wilaya ya Kilolo
AFISA Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Godfrey Mwita ameingia matatani akituhumiwa kuhusika na wizi wa magogo ya miti kwa ajili ya mbao,  uliotokea hivikaribuni katika msitu wa halmashauri hiyo wa Ng’ang’ange.

Wizi huo umeelezwa na halmashauri hiyo kusababisha hasara inayokadiriwa kuwa kati ya Sh Milioni 45 na 60.

Akikataa kuizungumzia tuhuma hiyo, Mwita ambaye bado anaendelea na kazi katika halmashauri hiyo alisema; “suala hilo lipo kwa mkurugenzi wa halmashauri, mimi siwezi kuzungumza chochote waone wao.”

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ubald Wampembe alisema suala hilo lilishafikishwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na linaendelea pia kuchunguzwa na mkaguzi wa ndani wa halmashauri na vyombo vingine vya dola.

Akizungumzia kwa kina tuhuma hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Joseph Muhumba alisema baraza la madiwani litatoa tamko rasmi baada ya uchunguzi wake kukamilika.

Muhumba alisema halmashauri hiyo ilibaini kuwepo kwa uvunaji wa magogo bila vibali baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rukia Muwango hivikaribuni kuunda timu maalumu iliyokuwa na lengo la kuvikagua vyanzo vyote vya mapato vya halmashauri hiyo.

Moja ya chanzo kilichotembelewa na kukaguliwa, alisema, ni misitu mitatu ya halmashauri hiyo ya Lusinga, Ukumbi na Ng’ang’ange.

Alisema timu hiyo ilipofika katika msitu wa Ng’ang’ange ilishuhudia uharibifu mkubwa ulioelezwa na majirani na baadhi ya mashahidi wao kwamba umetokana na wizi wa magogo ya mbao.

Alisema uchunguzi wa awali wa tukio hilo uliofanywa na mkaguzi wa ndani umebaini kuwepo na taarifa mbili zinazohusiana na hujuma hiyo, kati yake moja ikimuhusisha afisa misitu huyo.

Taarifa mojawapo kwa mujibu wa Muhumba inaonesha sehemu kubwa ya miti inayolalamikiwa kuvunwa kinyemela; ilivunwa kati ya mwaka 2010 na 2011 huku taarifa nyingine ikionesha miti hiyo imevunwa kupitia vibali vilivyotolewa hivi karibuni na halmashauri hiyo.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi ya awali iiyofanywa na mkaguzi wao wa ndani, Mwita anatuhumiwa kutoa ruksa kwa watu waliopewa vibali vya kuvuna; kuvuna miti zaidi ya ile iliyoidhinishwa na hivyo kuisababisha halmashauri hiyo hasara hiyo.

“Kwahiyo tumeona kuna mkanganyiko, kwasababu wapo wanaosema msitu huo ulihujumiwa mwaka 2010 na 2011 na wengine wanasema ulihujumiwa kwa maagizo ya Mwita; tunataka kutenda haki, kwakuwa anatajwa ni lazima achunguzwe na ikibainika kweli atachukuliwa hatua na ikibainika sio kweli ataendelea na majukumu yake” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment