Monday, 5 May 2014

WANAFUNZI ACHENI KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUTAFUTA MARAFIKI WA NGONO

Wahitimu katika picha ya pamoja
Msambatavangu akitoa nasaha
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavanngu amewasihi wanafunzi wa kike kuacha kukimbilia ngono na kutumia mitandao ya kijamii kutafuta wapenzi wapya kama wanataka kutimiza ndoto zao za kimaisha.

“Wapo wenye ndoto za kuolewa mara tu baada ya kumaliza elimu ya msingi; sijui kimaisha wanajiweka katika kundi gani?” alisema.

Alisema urithi pekee kwa mwanafunzi wa kike ni elimu ambayo kama utachanganywa na ngono unaweza usitimie kwani mbali na mimba, magonjwa ya zinaa na Ukimwi yanaweza kuvuruga matarajio yake.

Aliyasema hayo kwenye mahafali ya 22 ya wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari  ya wasichana Iringa (Iringa Girls) yaliyofanyika shuleni hapo hivikaribuni.

Msambatavangu alisema wanafunzi wa kike wanatakiwa wajiamini, wajitambue na kufahamu wajibu wao ili wajikomboe kifkra na kiuchumi kabla ya kutimiza ndoto za maisha yao.

Msambavangu alisema baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwasaka wa udi na uvumba wasichana wa shule wakiamiani kufanya nao ngono ni salama pamoja na uwezekano wa kupata magonjwa ya kujamiiana na mimba.

Alisema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwepo kwa kiu kubwa ya kufikia mafanikio ya juu miongoni mwa wanafunzi wa kike lakini kwa baadhi yao kiu hiyo imekuwa ikikatizwa na wanaume wakware.

“Asilimia kubwa ya wazazi wanataka mtoto kike asome ili afikie ngazi kubwa kama ilivyo kwa viongozi wa kike walio madarakani lakini kwa tamaa ya fedha na anasa wengi wenu mmekuwa mkiishia njiani,” alisema.

Aidha amewataka kuacha tabia ya kutumia kwa muda mrefu mitandao ya kijamii kutafuta marafiki wa kiume kwa kubadilibadili picha zenye pozi za kutamanisha.

“Tumieni mitandao hiyo kwa mambo mnayoona yatawaongezea uelewa katika harakati zenu za kutafuta elimu kwa maisha yenu, acheni kutumia mitandao hiyo kwa mambo yasio na msingi,” alisema.

Katika harambee ya kuchangia ununuzi wa gari la shule hiyo linalokadiriwa kuwa na thamani ya Sh Milioni 25,  Msambatavangu alichangia Sh milioni 1.5 kati ya Sh milioni 4 .6 zilizopatikana.

Mkuu wa shule hiyo Joyce Msigwa aliwashukuru wazazi wa wanafunzi kwa michango yao itakayowezesha shule hiyo kukabiliana na changamoto kubwa ya usafiri.

Inapotokea dharula ikiwemo ya ugonjwa, Msigwa alisema wanafunzi wanakabiliwa na wakati mgumu kwasababu ya ukosefu wa usafiri.


“Tunaomba wadau mbalimbali, wazazi na makampuni mbalimbali watuchangie ili tupate gari litakalopunguza changamoto tulizonazo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment