Wednesday, 7 May 2014

TANAPA YAIANGUKIA TMF KUIBUA MTANDAO WA MAJANGILI

DSC_0304
Meneja Mahusiano TANAPA, Pascal Shelutete
DSC_0241
Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura
PAMOJA na juhudi kubwa zinazofanywa nana wadau wake za kukabiliana na majangili wakiwemo wa meno ya tembo, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linataka mtandao wa majangili nchini ufichuliwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Ili kuumaliza mtandao huo, TANAPA imeuangukia Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ili utoe fedha kwa wanahabari wanaoweza kuchunguza taarifa za uwepo wa mtandao huo.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari jijini Arusha Mei 3, mwaka huu, Meneja Mahusiano wa TANAPA, Pascal Shelutete alisema: “tunaomba TMF itoe fedha kwa wanahabari.

Alisema nafasi walionayo wanahabari katika kuchunguza na kuibua taarifa zilizojificha zinaweza kusaidia kuunasa mtandao huo na kutokomeza kabisa ujangili nchini.

“Ni muhimu wanahabari wakashirikishwa katika shughuli hii nyeti ya kulinda rasilimali za Taifa. TMF wanaweza kuwasaidia kwa kuzingatia mazingira ya kazi yenyewe, TANAPA tunaomba mlifanyie kazi hilo na mkifanya hivyo mtakuwa mmelisaidia sana Taifa,” alisema.

Akijibu ombi hilo, Mkurugenzi wa TMF, Ernest Sungura alitoa ufafanuzi wa taratibu wanazoweza kuzitumia wanahabari kuomba ruzuku ili wakafanye uchunguzi wa mambo hayo.

Utaratibu huo unataka mwanahabari awe na wazo la habari analotaka kulifanyia uchunguzi kwa kujaza fomu maalumu ya maombi na kisha kuiwasilisha TMF kwa njia ya mtandao au posta. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment