Thursday, 15 May 2014

TANAPA KUCHANGIA SHUGHULI ZA UCHUMI ZA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA HIFADHI ZAKE

Mwenyekiti wa Mbomipa, Phillip Mkumbata akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa TNAPA, Allan Kijazi (kulia)
KWA kupitia kitengo chake cha ujirani mwema, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) litaanza kuchangia shughuli za kiuchumi zinazofanywa na vijiji vinavyozunguka hifadhi za taifa nchini ili kutunisha mifuko yao.

“Mpango huu utawaongezea kipato wananchi wa vijiji hivyo na kuwawezesha kubadili maisha yao, kukuza utalii na kushiriki katika uhifadhi wa maeneo yaliyohifadhiwa,” Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi alisema.

Kijazi aliyasema hayo alipokwa akitoa taarifa ya jinsi kitengo hicho kinavyosaidia shughuli mbalimbali za maendeleo za vijiji hivyo kwa Mkuu wa Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP), Helen Clark.

Katika ziara yake ya siku nne aliyoifanya hivi karibuni hapa nchini, Clark alipata fursa ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruha na kupewa na taarifa mbalimbali zinazohusu hifadhi hiyo, TANAPA na jumuiya inayozunguka hifadhi.

“Haitoshi kuendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu kama ya elimu, afya na barabara kwa vijiji jirani; tuna haja ya kuangalia pia namna ya kuchangia fedha jitihada zao zinazolenga kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Katika ziara yake hiyo, Clark alisema vijiji vinavyounda jumuiya za usimamizi shirikishi wa maliasili (WMA) ni ufunguo wa vita dhidi ya ujangili na biashara yake haramu.

Akizungumza na wawakilishi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori na Maliasili Tarafa ya Idodi na Pawaga (MBOMIPA) alisema jitihada za jamii ni lazima ziungwe mkono katika mapambano hayo.

Mbomipa ni Jumuiya ya vijiji 21 vya tarafa hizo vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, vilivyokubali kutoa sehemu ya ardhi yao yenye vivutio vya wanyama wa aina mbalimbali wanaotoka katika hifadhi ya Ruaha kwa ajili ya matumizi bora na kwa faida ya vijiji hivyo na taifa kwa ujumla.

“Iko wazi” alisema, “kila mmoja katika jamii, wakiwemo wanawake, vijana na wazee wana wana mchango katika mipango endelevu na ya muda mrefu ya ulinzi wa wanyamapori katika maeneo yaliyo jirani na maeneo yaliyohifadhiwa,” alisema.

Ndani ya hifadhi hiyo alisema amefurahi kukukutana na askari wa hifadhi wanaopata mafunzo ya mara kwa mara kupitia  mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) na akasisitiza umuhimu wao wa kupambana na ujangili kwa kushirikiana na jumuiya nje ya hifadhi hiyo.

Alisema jitihada zinazofanywa na jumuiya hiyo ni lazima zipewe ushirikiano na misaada wanayotaka ili kuongeza vipato vyao na kusaidia shughuli za uhifadhi, utalii na huduma zao nyingine.

Awali Mwenyekiti wa MBOMIPA, Phillip Mkumbata alisema jumuiya hiyo ipo katika mazingira magumu ya kupambana na ujangili kwasababu ya ukosefu wa vitendea kazi na mafunzo.

“Tunafahamu wajibu wetu katika kukabiliana na ujangili na kulinda maeneo yetu jirani na hifadhi, lakini tuna changamoto ya ukosefu wa magari ya doria, silaha na mafunzo kwa skauti wetu,” alisema.

Akitoa mfano alisema, changamoto ya ukosefu wa vifaa na mafunzo ulisababisha zaidi ya tembo 10 wauawe na majangili katika eneo lao la hifadhi katika kipindi cha mwaka jana pekee.

Pamoja na misaada wanayohitaji, Mratibu wa SPANEST, Godwell Olle Meing’ataki alisema mradi wao unashirikiana na MBOMIPA kuimarisha matandao wa maeneo yaliyohifadhiwa.

Kwa kupitia UNDP, Meing’ataki alisema sensa iliyofanywa katika ukanda wa Ikolojia wa Ruaha-Rungwa inaonesha Tembo wamepungua kutoka 31,625 mwaka 2009 hadi 20,090 mwaka jana.

Alisema kwa kupitia mradi huo, wanayo mipango mingi itakayosaidia kupata mpango kabambe wa kukabiliana na ujangili nchini.


UNDP kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) inafadhili mradi wa SPANEST.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment