Tuesday, 20 May 2014

PROFESA MSOLLA ACHANGIA UJENZI WA KANISA

Profesa Msolla akikabidhi mchango wake kwa Mchungaji wa KKKT Usharika wa Ndengisivili, Damas Chavalla
MBUNGE jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla ametoa Sh 150,000 kama mchango wake kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Ndengisivili, wilayani Kilolo.

Wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa kanisa hilo, waumini zaidi ya 120 wa usharika huo wanaabudu katika jengo la muda lililojengwa kwa tope huku likiwa limeezekwa kwa nyasi.

Profesa Msolla alitoa mchango huo hivikaribuni alipofanya ziara ya kijimbo katika kijiji hicho kwa lengo la kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka uliopita.

Mchango huo kwa mujibu wa Mchungaji wa Usharika huo, Damas Chavalla utasaidia kununua sehemu bati ziatakazotumika kuuzekea kanisa hilo.

Mchungaji Savalla alisema ujenzi wa kanisa hilo unaendelea kwa nguvu za waumini, wadau na KKKT Dayosisi ya Iringa.

“Mei 30 Baba Askofu Mdegella atatutembelea ili aone maendeleo ya ujenzi huu; katika ziara yake hiyo ataitumia kuhamasisha waumini na wadau wengine kutuchangia zaidi,” alisema.

Alisema ujenzi wa kanisa hilo litakalokuwa la kudumu ulianza Desemba mwaka jana na unatarajia kukamilika wakati wowote mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema kukamilika kwa kanisa hilo kutaleta furaha kwa waumini wake kwa kuzingatia kwamba; “tunapata kero kubwa wakati wa masika, jengo tunalotumia sasa ni la nyasi, wakati wa kipindi hicho huwa linavuja sana na kuvuruga utaratibu wa Ibada.”

Alisema usharika pia unahitaji usafiri utakaowawezesha kutoa huduma ya kutembelea vitongoji vya kijiji hicho na kurahisisha ushiriki wa mikutano ya kijimbo.

Kijiji cha Ndengisivili kipo zaidi ya kilomita 70 kutoka mjini Iringa yaliko makao makuu ya KKKT Dayosisi ya Iringa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment