Thursday, 8 May 2014

MAZISHI YA GERVAS KALOLO WA CHADEMA KUFANYIKA ALHAMISI YA LEO, ALIANDALIWA AWE MWENYEKITI IRINGA MJINI

Gervas Kalolo enzi za uhai wake akiwa katika magwanda

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akimnadi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo kata ya Miyomboni
ALIYEKUWA  akiandaliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa Mjini, Gervas Kalolo (52) atazikwa leo Alhamisi majira ya saa nane mchana katika makaburi ya Mtwivilla, mjini Iringa.

Kalolo alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumanne jijini Dar es Salaam alikokuwa ameenda kwa shughuli zake binafsi.

Mwili wake uliwasili mjini hapa Jumatano asubuhi na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Iringa ukisubiri taratibu mbalimbali za mazishi yake zinazotarajia kuhusisha viongozi mbalimbali wa kisiasa wa ndani nan je ya mkoa wa Iringa.

Taarifa za kifo chake zimepokelewa kwa masikitiko makubwa na wakazi wa mji wa Iringa na vitongji vyake waliomfahamu Kalolo kama msema kweli aliyekuwa haogopi mtu yoyote.

Kabla ya kujiunga na Chadema, Kalolo alikuwa diwani wa kata ya Miyomboni mjini Iringa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kati ya mwaka 2005 na 2010.

Alikikimbia chama hicho na kujiunga na Chadema mwaka 2010 baada ya kuangushwa na marehumu Marium Nyanginywa katika kura za maoni za CCM za mwaka 2010. Nyanginywa alifariki dunia April 2011 ikiwa ni mwaka mmoja na nusu tangu achaguliwe kuwa diwani wa kata hiyo.

Septemba mwaka 2011, Kalolo alitupa tena karata yake katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani kata ya Miyomboni baada ya kugombea  nafasi hiyo kupitia chama chake kipya cha Chadema.

Pamoja na kuwa na mvuto mkubwa wa kisiasa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja Kalolo aliangushwa katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 2, 2011 na mfanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha na mwenyekiti wa sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.

Ilionekana kuwa ni jambo gumu kwa wanachama wa Chadema kumpoteza mtu mwenye sifa hizo katika chama hicho.

Mapema mwaka jana, baadhi ya wanachama wanaojipambambanua kwamba ni wa kundi la mabadiliko katika chama hicho walianzisha harakati za kumpigia debe ili awe Mwenyekiti wa Chadema, Iringa Mjini katika uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Wanachama hao walitaka kumpa nafasi hiyo inayoshikiliwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa, Mchungaji Msigwa kwa kile walichokuwa wakidai kumpunguzia mbunge huyo majukumu mengi aliyonayo.

Mbali na kuwa mbunge, Mchungaji Msigwa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema; majukumu yanayoelezwa kuwa mazito yanayomkosesha muda wa kushughulikia majukumu mengine ya chama ya Iringa Mjini.

“Tumepota kiongozi wa mfano, mpiganaji na mpambanaji aliyekimbia hila za CCM na kujiunga na Chadema,” alisema Mchungaji Msigwa wakati akitoa taarifa ya kifo hicho bungeni juzi.

Reactions:

2 comments: