Thursday, 29 May 2014

FRANK LEONARD APATA TUZO YA TANAPA

FRANK LEONARD (KULIA) NA MHARIRI WAKE JOSEPH LUGENDO KWA PAMOJA WAKIWA WAMESHIKILIA MFANO WA HUNDI YA SH MILIONI 1.5 LIYOTOLEWA KWA LEONARD KAMA  MOJA YA ZAWADI KATIKA USHINDI WAKE KATIKA TUZO ZA TANAPA

LEONARD AKIHOJIWA NA MWANDISHI NA MTANGAZAJI WA TBC BENNY MWAIPAJA

LEONARD  AKIWA NA WASHINDI WENGINE WA TUZO ZA TANAPA 2013, KATIKATI NI VEDASTO MSUNGU NA KULIA NI GERALD KITABU WA THE GUARDIAN
MWANDISHI wa magazeeti ya serikali (Dailynews na HabariLeo) mkoani Iringa, Frank Leonard ametwaa tuzo ya uandishi bora wa habari za utalii wa ndani   kwa mwaka 2013.

Leonard ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) amekuwa miongoni mwa wanahabari 10 nchini waliojinyakulia tuzo za uandishi bora wa habari za utalii na uhifadhi kwa mwaka 2013.

Amekuwa mshindi wa pili kwa upande wa magazeti katika tuzo hizo zinazotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Kwa ushindi huo Leonard ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa www.frankleonard.blogspot.com maarufu kama BONGO LEAKS amezawadia Sh Milioni 1.5, cheti na ziara katika hifadhi za Taifa mbalimbali zilizoko nchini katika hafla ya aina yake iliyofanyika katika hotel ya Belmonte jijini Mwanza.

Mshindi wa kwanza alikuwa Gelard Kitabu wa The Guardian aliyejinyakulia Sh Milioni 2, ngao, cheti na atapata safari ya kwenda nje ya nchi (moja kati ya nchi za SADC) kutembelea vivutio vya utalii.

Mshindi wa tatu kwa upande wa magazeti alikuwa Jackson Kalindimya kutoka Nipashe ambaye alikabidhiwa hundi ya mfano ya Sh Milioni moja na cheti.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Razalo Nyalandu, Mkurugenzi wa TANAPA, Allan Kijazi, Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC), Aboubakar Karsan na wageni mbalimbali.

Amepata tuzo hiyo ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu apokee tuzo zingine mbili za umahiri wa uandishi wa habari zinazotolewa kila mwaka na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Leonard alipata ushindi baada ya kuonesha umahiri katika kuandika habari za afya ya uzazi na afya ya uzazi kwa vijana.

Katika tuzo hizo Leonard alikuwa mshindi wa pili na kujinyakulia zawadi mbalimbali vikiwemo ving’amuzi viwili vya DSTV.

Katika tuzo hizo za TANAPA, kwa upande wa redio mshindi wa kwanza katika kipengele cha utalii wa ndani alikuwa David Lwenyagira wa Redio 5 ya Arusha aliyepata Sh Milioni 2, ngao na ziara ya utalii katika moja ya nchi za Sadc.

Mshindi wa pili alikuwa Humphrey Mgonja wa Redio SAUT FM ya Mwanza aliyepata Sh Milioni 1.5, cheti na ziara katika hifadhi mbalimbali hapa nchini; kutoka redioni hakukuwepo na mshindi wa tatu wa habari bora za utalii wa ndani.

Walioibuka washindi wa habari za utalii wa ndani kwa upande wa Televisheni ni Kakuru Msimu wa Star TV aliyekuwa mshindi wa tatu na Kasim Mdame wa Channel Ten aliibuka mshindi wa pili huku nafasi ya kwanza ikikosa mshindi.

Kwa upande wa habari za uhifadhi kwa magazeti, Salome Kitomri wa Nipashe aliibuka mshindi wa tatu, huku nafasi ya pili na ya kwanza zikikosa washindi.

Kwa upande wa Televisheni, mshindi wa kwanza alikuwa Vedasto Msungu wa ITV, wa pili Raymond Nyamwihura wa Star TV, huku nafasi ya tatu ikikosa mshindi.

Zawadi zilizotolewa kwa washindi wa habari za uhifadhi hazikuwa na tofauti na zile zilizotolewa kwa washindi wa habari za utalii wa ndani wa magazeti, redio na televisheni.

Baada ya washindi hao kukabidhiwa zawadi hizo, wakiwa pamoja na wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo mbalimbali vya habari Mei 28 walitembelea hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Saanane jijini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment