Wednesday, 9 April 2014

WANAOZUNGUKA HIFADHI ZA TAIFA WATAKIWA KUWA NA MIPANGO BORA YA MATUMIZI YA ARDHI


Mratibu wa mradi wa SPANEST, Godwell Meing'ataki akitoa maelezo ya umuhimu wa mafunzo hayo

Katibu Tawala Msaidizi, Adam Swai akifungua mafunzo hayo
Washiriki wakiwa darasani
Washiriki wengine
washiriki
wakufunzi wa mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo hayo katika picha ya pamoja
ILI kunusuru rasilimali zinazoendelea kupotea katika hifadhi za Taifa, halmashauri za wilaya zinazozunguka maeneo hayo zimetakiwa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa, mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umeanza kutoa mafunzo hayo kwa watendaji wa halmashauri zinazozunguka hifadhi za kusini.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Meing’ataki alisema mafunzo hayo ya siku tano yanahusisha watendaji kutoka halmashauri za wilaya ya Mbeya, Wanging’ombe, Makete, Chamwino, Katavi na Iringa.

“Na wawakilishi kutoka hifadhi ya Ruaha, Mikumi, Udzungwa na Kitulo; na mapori ya kiba ya Rungwe, Mpanga Kipengele na Rungwa, Mhesi na Kizigo,” alisema.

Meing’ataki alisema halmashauri zinazozunguka hifadhi za Taifa zinatakiwa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepukana na migogoro inayopelekea baadhi ya wananchi wake kuvamia kwa matumizi yao maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa.

“SPANEST tunaamini tunachofanyakifanya kwenu kwa siku hizi tano hakitakuwa na umuhimu kama hakitaleta matokeo yoyote chanya baada ya kumaliza mafunzo haya,” alisema.

Akifungua mafunzo hayo jana, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Adam Swai alisema ardhi ni rasilimali ya msingi; ili kukidhi mahitaji yake hapana budi watumiaji wake wae na utaratibu na mipango itakayoathiri wengine.

Mwakilishi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Jarome Nchimbi ambaye ni mkufunzi wa mafunzo hayo alisema sheria ya mipango ya Matumizi ya Ardhi Namba 6 ya mwaka 2007 imeweka misingi ya kupanga matumizi hayo ya ardhi.

Alisema Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ni utaratibu wa kutathimini na kupendekeza namna mbalimbali za uhifadhi na matumizi ya maliasili au rasilimali ili kuinua uchumi wa Taifa na kuondoa umasikini.

Alisema katika mafunzo hayo, washiriki watajidiliana tishio dhidi ya viumbe hai vilivyohifadhiwa na matumizi bora ya ardhi kama njia muafaka ya kukabiliana na migogoro ya ardhi.

Mengine ni sera na sheria zinazosimamia matumizi bora ya ardhi, mipango ya kina ya usimamizi wa ardhi, mbinu za usuluhishi wa uatatuzi wa migogoro ya mipaka, tathmini shirikishi ya matumizi ya ardhi na mipaka na hali halisi ya matumizi ya ardhi ya kijiji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment