Wednesday, 30 April 2014

NYANYA YA ILULA HATARINI KUPOTEZA SOKO, YADAIWA KUWA NA MADHARA KWA MTUMIAJI

Nyanya ya Ilula
NYANYA inayozalishwa kwa wingi wilayani Kilolo mkoani Iringa iko katika hatari ya kukosa soko la ndani kwasababu ya kuharibiwa ubora wake.

Matumizi yasio kubalika ya dawa zinazotumiwa wakati wa mchakato mzima wa uzalishaji yameelezwa na afisa kilimo wa wilaya hiyo, Michael Mwaisondole kuhatarisha afya za mlaji wake.

Mwaisondole amesema Malawi ni moja ya nchi za jirani iliyokuwa ikinunua kwa wingi nyanya hiyo lakini imepiga marufuku uingizaji wake.

Baada ya kupima na kubainika ikiwa na aina nyingi ya dawa zinazoweza kumsababishia mlaji madhara, serikali ya nchi hiyo iliwahi kuteketeza shehena kubwa ya nyanya hiyo iliyoingizwa kwa matumizi mbalimbali nchini humo.

Afisa Kilimo huyo amesema wakiamini watapata matokeo ya haraka, baadhi ya wakulima wamekuwa wakidhibiti magonjwa mbalimbali yanayozikumba nyanya zikiwa shambani kwa kuchanganya na kupulizia aina tofauti za dawa kwa wakati mmoja.

Akitoa mfano alisema dawa aina ya Ridomil, Mancozes na Dithane M45 zinazotumika kudhibiti ukungu, zimekuwa zikichanganywa kwa pamoja na kutumiwa kwa wakati mmoja badala ya mkulima kutumia moja ya aina hizo za dawa kama atakavyoshauriwa na mtaalamu.

Alisema wakitafuta matokeo ya haraka kwa kudhibiti wadudu waharibifu wa zao hilo, baadhi ya wakulima wamekuwa wakichanga dawa aina ya sumicidin, carate, rogo na Rincomil na kunyunyiza kwa mimea hiyo.

“Matokeo yake, badala ya kufanya kazi iliyokusudiwa sumu inayotumika kutengeneza dawa hizo hufyonzwa ndani ya nyanya na baadaye kuleta madhara kwa mlaji,” alisema bila kutaja madhara hayo japokuwa alisisitiza kuwa ni ya muda mrefu.

Aliwataka wakulima wa zao hilo kubadilika ili kuliongezea thamani na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment