Tuesday, 22 April 2014

MZEE WA MIAKA 61 AKATWA NYETI ILEJE

Majirani wakimuhudumia majeruhi
Mbeya Yetu. Mkazi wa Kijiji Mapogolo wilayani Ileje, London Haonga (61), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya watu wanaodaiwa kuwa watatu kumkata sehemu za siri usiku wa kuamkia juzi.

Haonga alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni baada ya kupata huduma ya kwanza kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ileje alikofikishwa akiwa taabani.

Akiwa Hospitali ya Rufaa, jana hiyo mzee huyo hakuweza kusimulia lolote, lakini wauguzi wa Wodi ya Kwanza alikolazwa walisema hali yake inaendelea vizuri ingawa alikuwa na maumivu makali.

“Wamemkata sehemu zote za siri zikiwamo korodani,’’ alisema muuguzi, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Akizungumza kwa simu, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mapogolo, Cosmas London alisema Haonga alipatwa na mkasa huo saa 2.30 usiku wa kuamkia juzi baada ya watu wawili kumvamia njiani na kumfunga kitambaa na hatimaye kumkata sehemu zake za siri.

Alisema alipiga yowe kuomba msaada na majirani walifika na kutoa msaada wa kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Ileje huku wakiwasaka watuhumiwa wa tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema jeshi lake linaendelea na upelelezi na kuwasaka wahusika.

Msangi alisema taarifa za awali zinawahusisha ndugu wa Haonga na kwamba upelelezi unaendelea.

Kamanda Msangi alitoa wito kwa jamii kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi na kwamba wanapokuwa na migogoro ni vyema kutatua kwa njia ya mazungumzo ili kuleta amani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment