Monday, 21 April 2014

MCHUNGAJI MSIGWA AKUTANA NA WASHIKAJI ZAKE KIJIWENI KWAKE IRINGA, AFAFANUA KILICHOWATOA BUNGENI NA UWEZEKANO WA KURUDI KWENYE MEZA YA MAJADILIANOMbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akisisitiza jambo, huku washikaji zake wakimsikiliza


Ndio, tunaweza kukaa meza ya majadiliano kama watakuwa tayari tujadiliane namna ya kuboresha kile kilichopo kwenye rasimu

Serikali tatu zinawezekana kama zile zinazoonekana kama dosari zitaboreshwa
MBUNGE wa Bunge la Katiba, Mchungaji Peter Msigwa leo amekutana na washikaji zake katika kijiwe chake cha miaka yote, NSSF Iringa na kusaidia kutoa ufafanuzi wa mambo kadha wa kadha yaliyojili katika bunge hilo.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema wako tayari kukaa meza ya majadiliano baada ya kususia vikao vya bunge hilo kama majadiliano katika bunge hilo yatazingatia kile kilichomo kwenye rasimu ya Katiba.

Hivi karibuni wabunge hao waliamua kususia vikao vya bunge hilo kwa kile walichosema hawatendewi haki, wanatukanwa na kuzomewa pale wanapotoa michango yao.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alihitimisha uchangiaji wake uliopelekea wabunge hao kutoka nje baada ya kusema: “Ukawa hatuwezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.”

Baada ya kauli hiyo aliondoka akifuatiwa na Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wao kutoka nje ya Bunge.

Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, DP na NCCR-Mageuzi na wajumbe 25 kutoka kundi la 201 wameahidi kuzunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara kuwaleza wananchi kilichotokea.

Mchungaji Msigwa alisema CCM na serikali wana hofu ya kukosa madaraka kama watanzania wataridhia mapendekezo ya serikali tatu yaliyotolewa na Tume ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.

“Wabunge wanaowaunga mkono wameacha kujadili kilichomo katika rasimu hiyo ambayo ni muongozo wa uundaji wa katiba mpya unaotokana na maoni ya wananchi, wanatoa mapendekezo mapya,” alisema.

Alisema Rais Jakaya Kikwete na taasisi zake zote walitoa maoni yao wakati Tume hiyo ikikusanya maoni ya wananchi nchi nzima lakini chakushangaza alikuja na maoni mapya wakati akizindua rasmi shughuli za bunge hilo.

“Kimsingi bunge limehama kutoka kwenye yale yaliyomo kwenye rasimu na sasa tunajadili maoni ya Rais Kikwete aliyoyatoa baada ya muda wa kufanya hivyo kwisha,” alisema.

Mchungaji Msigwa alisema muundo wa serikali unaozungumzwa katika rasimu hiyo ni wa serikali tatu na akashangaa badala ya wajumbe kujadili namna ya kuboresha mapendekezo hayo, wanajadili mapendekezo mapya ya serikali mbili.

“Ukiangalia Ilani ya Chadema tulizungumzia serikali za majimbo, Ilani ya CCM inazungumza serikali mbili na vyama vingine navyo vina mapendekezo ya muundo wa serikali,” alisema.

Alisema pamoja na mitazamo ya vyama hivyo katika muundo wa serikali, Tume imekuja na mapendekezo ya serikali tatu katika rasimu hiyo na ndiyo inayotakiwa kujadiliwa.

“Badala ya wajumbe kuzungumzia namna tunavyoweza kuboresha mapendekezo hayo ya serikali tatu bila kuhatarisha muungano tulionao, tunazozana kwa maoni mapya,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment