Thursday, 24 April 2014

MAJANGILI WATEKETEZA MISITU YA ASILI IRINGA VIJIJINI, VIONGOZI WA VIJIJI WATUHUMIWA, KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YAITWA


Diwani Francisca Kalinga amewataja viongozi wanashirikiana na majangili

Uokotaji kuni katika misitu ya asili huenda sambamba na ukataji wa miti hiyo kwa matumizi mengine
Gunia za mkaa, zilikutwa ndani ya msitu wa Nyang'oro zikisubiri kusafirishwa
HALMASHAURI ya wilaya ya Iringa imeahidi kuishirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Iringa kukabiliana na ujangili wa miti ya asili unaosababisha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Madiwani wa halmashauri hiyo wamesema ujangili huo  umekethiri katika tarafa za Idodi, Pawaga, Isimani na Kalenga.

Wamesema skauti wanaofanya doria kwenye misitu ya asili wanashindwa kukabiliana na majangili hao kwasababu wana mfumo dhaifu wa ulinzi unaotumia silaha duni kama mapanga na marungu.

“Skauti wetu wanatumia virungu na mapanga wakati majangili wanatumia mishale na bunduki, katika mazingira hayo hakuna skauti anayeweza kuwa tayari kupoteza maisha yake,” alisema diwani Pascal Mwano.

Diwani mwingine wa halmashauri hiyo Phillemon Temaigwe alisema miti inayokatwa ni ile ya mbao na inayotumiwa kwa ajili ya uchomaji wa mkaa.

Alisema bidhaa zinazotoka na miti hiyo (mkaa na mbao) hazizalishwi kwa matumizi ya watu wa vijiji husika bali usafirishwa hadi mijini kwenye wateja wengi.

Alisema kuendelea kupambana na ukataji miti ovyo kwa kuweka vizuizi barabarani hakusaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwasababu wahusika hutumia mbinu nyingi kuruka vihunzi ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa.

“Dawa ya uhakika ya kulinda rasilimali zetu ni kwa halmashauri kuziongezea nguvu vijiji ikiwa ni pamoja na kutumia askari wenye silaha kali kuwasaska, kuwakamata na kuwatia katika mikono ya sheria majangili hao,” alisema.  

Diwani Francisca Kalinga alisema pamoja na udhaifu uliopo, baadhi ya viongozi wa vijiji wakiwemo wenyeviti wanashirikiana na majangili kuhujumu rasilimali hiyo muhimu.

Mbele ya watendaji wa halmashauri hiyo, Kalinga alitoa mfano kwa kuwataja baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Usolanga kwamba wanashirikiana na majangili kukwamisha jitihada za taifa za kulinda rasilimali hiyo.

“Wakati wa msako viongozi hao huwataarifu wahusika hao ili watoroke; pamoja na hujuma hiyo viongozi hao hawachukuliwi hatua zozote, wanafahamika na tumewataja mara nyingi,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili na Mazingira wa kijiji cha Mbweleli, Hussein Mwanagomba hivi karibuni alisema miti aina ya Miwondo na Mihavava iliyopo katika msitu wa asili wa Nyang’oro Kaskazini ipo hatarini kutoweka ikiwa ni matokeo ya kukithiri kwa shughuli za uchomaji mkaa na upasuaji mbao usiofuata kanuni na taratibu.

Alisema uchomaji mkaa na upasuaji mbao ndio shughuli ya uhakika inayotegemewa na wananchi wa kijiji hicho kwa ajili ya kujipatia kipato.

Mwanagomba alisema ukame uliokithiri katika eneo hilo umeondoa matumaini ya wananchi wa kijiji hicho kutegemea kilimo kwa ajili ya maisha yao.

“Tumethiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi, mvua hazinyeshi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo, na bwawa la Mtera ambalo sehemu yake lipo katika kijiji chetu halina samaki wa kutosha kama zamani na hivyo kuathiri shughuli za uvuvi,” alisema.

Alisema wananchi walio wengi wamekimbilia msituni ambako huchoma mkaa na kukata miti kwa ajili ya kupasua mbao kama mbinu mbadala ya kukabiliana na hali ngumu ya uchumi.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo aliomba serikali iangalie uwezekano wa kujenga bwawa lingine ambalo maji yake yatatumiwa na wananchi wa kijiji hicho kwa kilimo cha umwagiliaji.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Patrick Galwike alikiri changamoto hiyo kubwa na akahidi kuipeleka kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ili iweze kufanyiwa kazi kwa ufanisi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment