Saturday, 19 April 2014

KWANINI CCM INAPOTEZA MVUTO KWA VIJANA?

Frank Makakuro akihoji sababu ya CCM kupoteza mvuto kwa vijana
Profesa Msolla akitoa ufafanuzi
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa Profesa Msolla katika kijiji cha Kilolo ulioofanyika darasani kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Iringa
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kilolo kimeanza kuhoji sababu za vijana wengi kukacha kujiunga na chama hicho.

Frank Makakuro aliuliza katika moja ya mikutano ya kila mwaka ya Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla ya kukagua shughuli za maendeleo ya jimbo lake iliyofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Kilolo sababu za vijana kutojiunga na chama hicho.

“Mheshimiwa mbunge unajua kwanini vijana wengi hawajiungi na CCM, unajua kwanini wanakimbilia vyama vya upinzani, unajua athari zake kwa CCM?” 

Makakuro, kijana aliyejinasubi kukipenda kwa moyo wake wote chama hicho alisema; kwasababu hakuna vikao, hakuna mikutano na hakionekani kwa vijana, kinapoteza mvuto kwa kundi hilo muhimu katika siasa za nchi.

Alisema katika mikutano mingi ya chama hicho ikiwemo inayofanywa na mbunge huyo mara kwa mara, idadi kubwa ya watu wanaohudhuria ni wale wenye umri wa zaidi ya miaka 40.

“Kuna vijana wachache, lakini wengi wanaohudhuria mikutano ya chama changu CCM ni akinamama na akina baba wenye umri wa zaidi ya miaka 40, kwaninini?” aliuliza.

Akijibu swali hiyo Professa Msolla aliutaka uongozi wa CCM wa wilaya hiyo ueleze kwa wananchi ukweli kuhusiana na madai hayo na kile unachofanya kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo alisema CCM ni chama chenye demokrasia ya kweli inayojidhihirisha kwa kuwa na viongozi wa rika tofauti katika ngazi zake mbalimbali za uongozi.

“Ukienda kwenye umoja wa vijana-UVCCM, utakuta vijana wanavyochanua, ukienda kwa wanawake UWT- utakuta wanawake walivyo wengi; na ukirudi katika chama kuna mchanganyiko mkubwa wa makundi ya vijana, akinababa na wanawake na ndio maana kinaongoza kwa kuwa na wanachama wengi kati ya vyama vyote vya siasa nchini,” alisema.

Alisema demokrasia ya kweli katika chama hicho ndiyo inayowezesha pia uwepo wa mchanganyiko wa kutosha katika nafasi zingine za uongozi ndani ya serikali na zile za kuchaguliwa na wananchi.

“Angalia chama kilivyo na idadi kubwa ya wabunge vijana, wenye umri wa kati na wazee; mchanganyiko huo ni muhimu sana kwasababu ya kubadilishana uzoefu,” alisema.

Alisema ili mchanganyiko huo uwe na tija zaidi alishauri kusiwe na pengo kubwa baina yao, vinginevyo kunaweza kuleta matatizo katika chama na nchi kwasababu ya umuhimu wa kila upande kwa upande mwingine.

Katibu wa CCM wilaya ya Kilolo, Raphael Mahumba alisema katika mkutano huo pamoja na uwepo wa vijana wengi ndani ya CCM, mikakati ya kuwasajili wengi zaidi katika chama hicho imeanza kufanywa.

“Ndio; kuanzia mwezi ujao tutafanya mikutano katika vijiji vyote vya jimbo hili na mbali na mambo mengine ya kukijenga chama, kazi yetu kubwa itakuwa kuwashawishi vijana wasio wanachama wetu kujiunga nasi,” alisema.

Alisema chama hicho kinafahamu nguvu na umuhimu wa vijana katika shughuli za kisiasa na maendeleo ya taifa hivyo akatoa mwito kuwaunga mkono.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment