Wednesday, 16 April 2014

HESABU YA VIJIJI VITATU VYATEKETEA KILA MWAKA KWA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Mkurugenzi wa Evidence for Action, Tanzania, Craig John Ferla
Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya

baadhi ya walengwa wa mradi

wanahabari wakifuatilia mada


WANAHABARI 48 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, wamepata mafunzo ya namna ya kuandika habari za afya ya uzazi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa hotel ya Lion, jijini Dar es Salaam kwa uratibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Kwa kupitia Kampeni ya Mama Ye!, UTPC inashirikiana na asasi ya Evidence for Action yenye makao yake makuu nchini Uingereza kutekeleza mradi huo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanahabari kukuza uwajibikaji katika kulinda afya ya mama, mzazi na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na ujauzito.

Mkurugenzi wa Evidence for Action, John Craig Ferla aliwaambia wanahabari walioshiriki mafunzo hayo kwamba takwimu za Shirika la afya Duniani (WHO) linaonesha  wajawazito 8,500 pamoja na watoto wachanga 50,000 hufariki dunia kila mwaka hapa nchini kutokana na matatizo yanatokanayo na ujauzito.

Akizungumzia idadi ya wajawazito wanaofariki kila mwaka alisema taifa linapoteza wastani wa watu wanaoishi katika vijiji vitatu kila mwaka. Kwa wastani kijiji kimoja kina watu kati ya 1,500 na 3,000.

Alisema watu hao wanakufa si kwasababu Mungu amewapenda sana na kuamua kukatisha uhai wao ila ni kwasababau ya kukosekana kwa huduma bora za afya katika maeneo yao.

Mshauri wa mradi huo nchini, Dk Moke Magoma alisema Lengo la Millenia namba tano na nne linataka vifo vya wajawazito na watoto vipungue kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.

Alisema maisha ya akina na mama na watoto wanaweza kuokolewa kama kutakuwa na huduma bora za afya kwasababu ushahidi wa kitaalamu unaonesha vifo vingi vitokanavyo na matatizo ya uzazi vinazuilika.

Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya alisema katika mafunzo hayo kwamba  wanahabari wana nafasi ya kipekee katika kampeni hiyo.

Alisema wanahaabari ni watetezi wa maslai ya jamii wenye wajibu wa kuhakikisha mikakati inayotengenezwa na kuzinduliwa kwa mbwembwe haiishi kwenye makabati ya viongozi wa wahusika.

“Wanahabari tunaweza kuibua hisia na changamoto na tukasaidia kuhamasisha jamii na serikali zao kufikia  mafanikio ya malengo waliojiwekea,” alisema.

Alisema kwa kupitia UTPC, wanahabari nchini kote wanaweza kufika katika maeneo yenye athari kubwa zaidi za upatikanaji wa huduma (vijijini) na kuhamasisha jamii kuchukua hatua.

Katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, Simbaya alisema kila mtu anawajibu wa kuchukua hatua.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment