Wednesday, 23 April 2014

GHOROFA ZAONGEZEKA MJINI IRINGA NI PAMOJA NA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA UJENZI KATIKATI YA MJI KUWEKWA KIPORO

Katikati ya mji wa Iringa panavyoonekana hivi sana, majengo ya ghorofa yanazidi kuchipua
ZAIDI ya miaka minne iliyopita, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa iliamua kuweka kiporo utekelezaji wa sheria zinazohusiana na mipango miji.

Moja ya eneo linalozungumzwa katika utekelezaji wa sheria zinazohusiana na mipango miji ni ujenzi wa nyumba za ghorofa katikati ya miji, ukiwemo mji wa Iringa.

Sura ya 378 ya Kifungu cha 35 cha Sheria hiyo ya mipango miji ya mwaka 1961 inazuia kufanya ukabati mkubwa wa nyumba za kawaida zilizopo katikati ya mji na badala yake inataka zijengwe nyumba za ghorofa.

Katika moja ya vikao vyake vya muda mrefu, Baraza la Madiwani la Manispaa ya Iringa liliazimia katika kutekeleza sheria hizo, kutoruhusu kufanya ukarabati mkubwa wa majengo katika ya mji wake.

Na kwamba anayetaka kufanya hivyo atawajibika kujenga ghorofa, vinginevyo hakuna kibali kitakachotolewa kwa ukarabati wa kawaida; lengo likiwa kubadilisha mandhari ya mji wa Iringa ili uwe wa kisasa wenye hadhi inayofanana na miji mingine.

Katika kukwepa utekelezaji wa kile ilichoazimia, halmashauri hiyo iliamua kuweka kiporo utekelezaji wa sheria ya mipango miji na kwa kupitia maamuzi yaliyofanywa na Baraza lake la madiwani ilianza kutoa vibali kwa watu wanaotaka kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba zao za kawaida zilizopo katikati ya mji.

Wanaopata vibali hivyo, hasa kwa wanaokarabati kwa shughuli za biashara, wanatakiwa baada ya miaka mitano baada ya ukarabati wao wabomoe na kujenga ghorofa.

Mfano mwaka 2009, mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa mjini Iringa maarufu kwa jina la Mambo Leo alifikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria hiyo na kuamuliwa kulipa faini ya Sh 300,000 kama asilimia mbili ya kuendeleza jengo lake lililoko Mshindo Iringa mjini kinyume na sheria.

Pamoja na faini hiyo, mahakama ilimpa miaka mitatu tu mfanyabiashara huyo ya kuendelea kulitumia jengo hilo kwa shughuli zake, na baada ya hapo aliagizwa abomoe na kujenga ghorofa, uamuzi ambao haujatekelezwa hadi hii leo.

Mwaka 2007, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Kasungu alizungumzia jinsi anavyokerwa na halmashauri hiyo, hususani idara yake ya ardhi na mipango miji kwa kuwa na udhaifu mkubwa wa kusimamia sheria za mipango miji.

Alipokuwa akizungumza na wanahabari ofisini kwake, mtandao huu unakumbuka jinsi Mkuu huyo wa Mkoa alivyonukuliwa akisema; “Pamoja sheria hiyo kutaka ujenzi wa nyumba za ghorofa ufanyike katikati ya mji pale nyumba za kawaida zinapobomolewa, imeendelea kushuhudiwa jinsi sheria hiyo inavyokiukwa.

Kasungu aliitoa kero hiyo, baada ya mmoja wa waandishi wa habari kuuliza hatua ambazo serikali inaweza kuzichukuwa kwa watu wanaovunja sheria hiyo.

Alisema idara zinazohusika na maendeleo ya mji huo, zimekuwa zikiruhusu kinyemela baadhi ya nyumba kubomolewa na kujengwa ovyoovyo kinyume na sheria hiyo.

Hata hivyo aliyekuwa, mwanasheria wa manispaa hiyo, Anna Ngowi alinukuliwa akisema pamoja na uzuri wake sheria mpya ya mipango miji inachochea ukiukaji wa utekelezaji wa sheria hiyo.
 
“Sheria ya zamani ilikuwa inazipa halmashauri mamlaka ya kutoa notisi ya siku 30 kwa watu wanaokiuka sheria hiyo, wasipobomoa kwa hiari yao majengo wanayoyaendelezwa au kujengwa upya kinyume na sheria, halmashauri zenyewe zilikuwa na nguvu ya kubomoa na kudai fidia kwa wahusika,” alisema.
 
Ngowi alisema sheria ya sasa inawazuia kubomoa mejengo yanayojengwa au kuendelezwa kinyume na sheria na badala yake inawataka waende mahakamani ili wapate idhini ya kufanya hivyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment